Serikali Yawakumbusha Watoa Huduma Migodini: Toeni Bidhaa Bora, Fursa Zidumu


 Mwandishi Wetu  Dodoma,

Watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa kwenye migodi ya madini nchini wametakiwa kuzalisha bidhaa bora, kuzingatia maadili ya kazi na kuwa waadilifu ili kujenga imani kwa kampuni za madini na kurahisisha utekelezaji wa Kanuni 13A ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini za mwaka 2018.

Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, CPA Venance Kasiki, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, wakati wa kikao kilichowakutanisha watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa kwenye migodi pamoja na wamiliki wa leseni za madini. Kikao hicho kililenga kutoa uelewa kwa wadau kufuatia marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania yaliyofanywa na Wizara ya Madini mwezi Septemba, 2025, yanayobainisha kuwa baadhi ya huduma na bidhaa zitolewe na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100.

CPA Kasiki amesema Serikali, kupitia Tume ya Madini, imeendelea kufanya maboresho ya Kanuni hizo ili ziendane na matakwa ya Sheria ya Madini na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini. 

Amefafanua kuwa mwezi Novemba, 2025, Tume ilitoa tangazo la orodha ya bidhaa na huduma zinazoweza kutolewa na Watanzania kwa umiliki wa asilimia 100, hatua iliyotokana na marekebisho ya Kanuni yaliyofanyika Septemba, 2025.

Ameongeza kuwa Tume ya Madini itaendelea kutoa na kuhuisha orodha ya huduma na bidhaa hizo kwa nyakati tofauti, kulingana na mahitaji ya Kanuni, huku akiwahimiza watoa huduma kuchangamkia fursa zilizoongezeka kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyohitajika na kampuni za madini.

“Hapo awali, kampuni nyingi za madini zilikuwa zikiagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, hata huduma za usafiri wa wafanyakazi zilitolewa na wageni. Maboresho yaliyofanywa na Serikali yameongeza fursa kwa Watanzania; hivyo ni muhimu mkazingatia ubora ili kujenga uaminifu, kujipatia kipato, kuzalisha ajira na kuiwezesha Serikali kukusanya mapato stahiki,” amesisitiza CPA Kasiki.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha wadau wakati wa kutangaza huduma na bidhaa husika, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, kutatua changamoto za wadau na kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kukua kwa tija na uendelevu.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma kwenye Migodi (TAMISA), Japhet Mussa, amewataka watoa huduma kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa huduma na kusambaza bidhaa zenye ubora, badala ya kujikita katika uchuuzi.

“Tunaishukuru Serikali kwa hatua kubwa iliyochukua kuhakikisha watoa huduma wa ndani wananufaika na sekta ya madini. Rai yangu ni kuhakikisha tunazalisha na kusambaza bidhaa bora ili kudumisha ushindani na uaminifu,” amesema.

Naye Katibu Mtendaji wa Tanzania Chamber of Mines (TCM), Benjamin Mchwampaka, ameipongeza Tume ya Madini kwa hatua zilizopigwa katika kuimarisha Ushirikishwaji wa Watanzania na kwa ufafanuzi uliotolewa kuhusu tangazo la Novemba, 2025. 

Amesisitiza umuhimu wa Tume kuyafanyia kazi maoni na ushauri wa wadau ili kufanikisha utekelezaji wa Kanuni hizo na kuimarisha maendeleo ya sekta ya madini nchini.




Post a Comment

Previous Post Next Post