SERIKALI KUHARAKISHA UJENZI WA VIWANDA VYA DAWA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza  mkakati mpya wa kuharakisha ujenzi wa viwanda vya dawa na bidhaa za afya nchini, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa afya wa Taifa, kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya uzalishaji wa dawa barani Afrika na duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao cha wazalishaji wa dawa na bidhaa za afya, Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, amesema uamuzi wa kujenga viwanda vya dawa si wa majaribio bali ni msimamo wa kimkakati uliokwishaamuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Mhe. Mchengerwa amesema Serikali imedhamiria kujenga mfumo imara wa uzalishaji wa dawa ndani ya nchi, akisisitiza kuwa usalama wa afya wa Taifa hauwezi kujengwa kwa kutegemea uagizaji wa dawa pekee bila kuwa na uzalishaji wa ndani wenye tija na uhakika.

Amesema uzalishaji huo unapaswa kuzingatia viwango vya kimataifa, hususan viwango vya WHO-GMP, akibainisha kuwa viwango hivyo si anasa wala mapambo bali ni kigezo muhimu cha kuingia kwenye soko la kimataifa la dawa.

Katika hotuba yake, Waziri Mchengerwa amesema changamoto kubwa ya Tanzania katika biashara ya kimataifa ya dawa si ukosefu wa soko, wataalamu au fursa za uwekezaji, bali ni kushindwa kukidhi viwango vinavyotambulika kimataifa.

Akinukuu takwimu za mwaka 2023, amesema Tanzania iliuza dawa nje ya nchi zenye thamani ya chini ya dola milioni moja, wakati Kenya iliuza dawa zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 140, hali aliyoeleza kuwa inadhihirisha tofauti kubwa ya viwango na ushindani.

Ili kuondoa vikwazo vya kiurasimu, Waziri amesema Serikali imeanzisha mfumo wa uharakishaji wa uwekezaji unaojulikana kama Green-Lane Approval System chini ya Pharmaceutical Investment Acceleration Programme, sambamba na kuunda Kikosi Kazi cha Pharmaceutical Investment Acceleration Taskforce (PIAT).

Amesema mfumo huo utawezesha wawekezaji kupata maamuzi ya haraka, wazi na yanayotabirika, huku Serikali ikiondoa urasimu wa mizunguko mirefu uliokuwa ukikwamisha uwekezaji katika sekta ya dawa.

Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza kuwa tayari imetoa Tangazo la Expression of Interest (EOI) kwa ajili ya uwekezaji katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya, likilenga kuvutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa pamoja na kuhamasisha ubia wa kimkakati. Mwisho wa kuwasilisha maombi ya EOI umetajwa kuwa ni Machi 2, 2026.

Mhe. Mchengerwa amewataka wazalishaji wa ndani kuwekeza zaidi katika ubora, teknolojia na mifumo ya viwango, akisisitiza kuwa msaada wa Serikali utaelekezwa kwa viwanda vinavyokidhi au vinavyoonesha dhamira ya wazi ya kufikia viwango vya kimataifa.

Aidha, ametoa onyo kali dhidi ya jitihada zozote za kuhujumu au kuchelewesha kwa makusudi ajenda ya maendeleo ya viwanda vya dawa, akisisitiza kuwa ajenda hiyo ni ya Taifa na inapaswa kuungwa mkono na wadau wote, huku akiwahimiza waingizaji wa dawa kuchukulia mabadiliko hayo kama fursa ya kuwekeza katika uzalishaji wa ndani kupitia ubia na uhamishaji wa teknolojia.


Post a Comment

Previous Post Next Post