
Na. Edmund Salaho -Arusha
Bodi ya Wakurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA INVESTMENT LTD – TIL) imezinduliwa rasmi leo Novemba 10, 2025 jijini, Arusha na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini – TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali George Marwa Waitara.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo Jenerali Waitara aliipongeza bodi hiyo na kuwataka kuimarisha uongozi wa kitaalamu katika usimamizi wa maendeleo ya kampuni hiyo.
“Bodi ya Wadhamini inawapongeza kwa kuchaguliwa kuongoza kampuni hii twendeni pamoja kusimamia kwa weledi na uwazi miradi yote itakayotekelezwa na Kampuni, tukaimarishe ushirikiano kati ya Kampuni, TANAPA, na wadau mbalimbali kwa misingi ya uwajibikaji, ubunifu na uadilifu.”
“Ni matarajio yetu kwamba mtaleta Ubunifu katika uwekezaji unaoleta tija, Ujenzi wa taswira chanya ya Kampuni katika sekta za umma na binafsi, pamoja na Utekelezaji wa miradi inayolingana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwemo falsafa ya uhifadhi endelevu na wenye tija kwa Taifa na jamii kwa ujumla” alisema Waitara
Naye, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA. Mussa Nasoro Kuji alibainisha kuwa Shirika linaendelea kutambua mchango mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi nchini na hususan kwenye eneo la uhifadhi na utalii nchini.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TIL, Mhandisi Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Kampuni imejipanga vilivyo katika kuleta mapinduzi katika ukandarasi huku ikijidhatiti kwa utaalamu wa hali juu, pamoja na vifaa vya kutekeleza kazi hizo za ukandarasi.
“TIL tunao wataalamu wenye elimu mbalimbali na uzoefu mkubwa katika kazi hizi za ukandarasi Kampuni inavyo vifaa vingi na vya kisasa. Tunaahidi kuchapa kazi yenye ubora wa hali ya juu”.
TANAPA INVESTMENT LTD (TIL) ni Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya TANAPA ilianzishwa kwa malengo makuu ya Kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya Shirika kwa gharama nafuu zaidi na Kutekeleza miradi nje ya Shirika kama kitega uchumi.
