Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amewasili rasmi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma na kuanza kutekeleza majukumu yake mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 5 Novemba, 2025 Ikulu Chamwino, Jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Johari alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua tena kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuendelea na majukumu ya kuishauri Serikali katika masuala yote ya kisheria.
“Nimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa kwangu na kuniteua tena kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuendelea kuishauri Serikali kama ilivyoainishwa katika Katiba na Sheria, Namshukuru sana Mhe. Rais.” Amesema Mhe. Hamza Johari
Katika hatua nyingine, Mhe. Johari amewashukuru Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidii na kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuboresha fikra zao katika utekelezaji wa majukumu yao kwakuwa Mhe. Rais amewaamini.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alionyesha kusitikishwa na matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani uliojitokeza katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
“Wanasheria sisi tuko mahiri na najua tutakuja na solution nzuri, ili tuweze kuishauri Serikali vizuri.”Anasema Mhe. Johari
Akitoa salamu za pongezi Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakimu Maswi, amempongeza Mhe. Hamza S. Johari kwa kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
*”Kwa Heshima na Taadhima tunapenda kutoa pongezi za dhati kwako wewe Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuaminiwa tena na kupewa Heshima kubwa ya kuendelea kulitumikia Taifa letu katika nafasi hii adhimu.”* Anasema Katibu Mkuu
Sambamba na hilo, Katibu Mkuu amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi huu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku akisema kuwa ni mtu sahihi katika nafasi hiyo.
*”Lakini pia namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuona kwamba wewe unastahili kuendelea kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Mujibu wa Sheria wewe ndio Kiongozi wa kwanza kuteuliwa na mhe. Rais.”* Anasema Bw. Maswi
Awali, akizungumza kwa niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole amemkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kueleza kuwa Watumishi wa Ofisi hiyo wako tayari kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kumpatia ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake .
Naye, Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester A. Mwakitalu amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuteuliwa tena na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ameahidi kuendelea kumpatia ushirikiano muda wowote atakapohitaji.
Vilevile, Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi amempongeza Mhe. Hamza S. Johari kwa kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake na huku akisema kuwa Ofisi yake itaendeleza ushirikiano ulipo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Zella Rwemanyila amemuahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuifikia na kuiishi kauli ya mbiu ya Weledi na Ubora.
Hafla hiyo fupi ya kumkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ofisini kwake Mtumba, Jijini Dodoma pia ilihudhuriwa na Naibu Katibu, Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Nchini, Bw. George Mandepo na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi.Alice Mtulo.
