JKCI YAPOKEA MASHINE YA KISASA KUBORESHA UANGALIZI WA WAGONJWA ICU

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Healthcare Tanzania, Sandip Datta msaada wa monita inayopokea taarifa za hali za wagonjwa zaidi ya 16 kwa wakati mmoja (Monitoring Central Station). Monitor hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 68 itasaidia kukusanya taarifa za hali za wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

Mkurugenzi wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Healthcare Tanzania Sandip Datta akimuonesha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge namna Monita ya kupokea taarifa za hali za wagonjwa zaidi ya 16 (Monitoring Central Station) inavyofanya kazi wakati kampuni hiyo ilipotoa msaada wa monita hiyo leo jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akisikiliza maelekezo ya jinsi  ya kutumia monitor inayopokea taarifa za hali za wagonjwa zaidi ya 16 (Monitoring Central Station) iliyotolewa msaada na kampuni ya Computech Healthcare Tanzania katika Taaasisi hiyo. Monitor hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 68 itasaidia kukusanya taarifa za hali za wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

Picha na JKCI

********

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea msaada wa monitor ya kisasa yenye uwezo wa kufuatilia taarifa za wagonjwa zaidi ya kumi na sita kwa wakati mmoja (Central Monitoring Station) waliolazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

Msaada huo wa monitor moja yenye thamani ya shilingi milioni 68 umetolewa leo jijini Dar es Salaam na kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Healthcare Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada walioutoa na kusema monitor hiyo itasaidia kuboresha huduma za uangalizi kwa wagonjwa waliolazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo alisema mashine hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa kuwa inafuatilia hali za wagonjwa wengi kwa wakati mmoja kwa njia za kidijitali.

 “Kupitia Central Monitoring Station hii wauguzi wataweza kufuatilia mapigo ya moyo, shinikizo la damu na umeme wa moyo wa wagonjwa kwa wakati mmoja. Teknolojia hii itarahisisha ufanyaji wa kazi, kupunguza changamoto za ufuatiliaji wa mgonjwa mmoja mmoja na kuongeza usahihi katika utambuzi wa matatizo ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge aliongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea na mpango wa kuhakikisha huduma zote za kitabibu zinakuwa za kidijitali ili kuboresha ufanisi na kupunguza matumizi ya nguvu kazi ya kibinadamu.

“Hivi sasa tunalenga wagonjwa wote wawe wanafuatiliwa kidijitali. Vifaa hivi vina akili bandia (AI) inayoweza kugundua mapema mabadiliko ya kiafya kwa mgonjwa na kusaidia kutoa huduma za haraka na zenye ubora zaidi”, alifafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Healthcare Tanzania Sandip Datta alisema msaada huo ni sehemu ya ushirikiano endelevu kati ya kampuni yake na JKCI katika kuboresa ubora wa huduma za afya nchini.

“Tumeamua kuleta teknolojia hii ya Central Monitoring Station ili kusaidia wauguzi na madaktari kufuatilia wagonjwa kwa urahisi zaidi. Hii ni hatua muhimu katika safari ya kidigitali ya sekta ya afya Tanzania”, alisema Datta.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya alisema monitor hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wauguzi katika kuhakikisha wagonjwa wote wanapata uangalizi wa karibu kupitia mfumo mmoja.

“Kwa sasa muuguzi mmoja anaweza kukaa kwenye kituo kimoja na kufuatilia wagonjwa zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Kifaa hiki kitaunganisha monitors zote za wagonjwa na kuonyesha taarifa zao sehemu moja, jambo litakaloongeza kasi na ubora wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa walioko ICU”, alisema Mallya.

Post a Comment

Previous Post Next Post