Elimu ya mbolea yaongeza hamasa kwa vijana wakulima


 Mwandishi Wetu,

Elimu ya matumizi sahihi ya mbolea inayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewaongezea ujasiri wa kuingia kwenye kilimo wakulima chipukizi hususan vijana.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki mara baada ya wataalamu wa kilimo wakiongozwa na Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi Levin Magere kumtembelea mkulima  Samiah Kulagawa anayejishughulisha na kilimo cha Nyanya katika Kijiji cha Kiromo Bumo, mkoani Pwani ili kujua maendeleo yake mara baada ya kupewa elimu hiyo.

“Nawashukuru sana Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kunionesha njia.” Hayo ni maneno ya shukrani ya mkulima kijana, Samiah Kulagawa, ambaye kwa mara ya kwanza anaanza safari yake ya kujikita kwenye uzalishaji wa mazao ya mbogamboga.

Samiah anasema, hatua yake ya kuingia kwenye kilimo inachochewa na elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea aliyopokea kupitia TFRA huku akibainisha kuwa, kabla ya mafunzo hayo hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa mbolea tofauti katika hatua mbalimbali za ukuaji wa mazao.

“Nawashukuru Wizara ya Kilimo kupitia TFRA kwa kunipatia elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kunisaidia kupata mbolea za kuanzia za kupandia hadi za kuzalishia. Wataalam wamekuwa wakinitembelea na kuniwezesha kuanza kilimo changu kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo,” anasema Samiah.

Anafafanua kuwa, safari yake bado ni changa, lakini ana matumaini makubwa kutokana na mwongozo wa kitaalamu anaoupata pamoja na mazingira wezeshi yaliyowekwa na serikali yakuwasaidia wakulima kulima kwa tija pamoja na kuweka ruzuku kwenye mbolea. 

Aidha, Samiah anatoa rai kwa vijana wenzake kuiona sekta ya kilimo kama nyenzo muhimu ya kujenga uchumi wao. “Natoa wito kwa vijana tuingie kwenye kilimo kwa sababu kilimo ni pesa. Na ili tuwe na tija, ni muhimu kutumia mbolea kwa usahihi katika uzalishaji wetu kama tunavyoelekezwa na wataalam,” anasema.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kuwawezesha vijana kujikita katika kilimo chenye tija kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora, elimu ya kitaalamu na huduma endelevu za ugani.




Post a Comment

Previous Post Next Post