ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA YAENDELEA KUTOLEWA MANISPAA YA SUMBAWANGA

 
Wakulima katika kata za Katumba Azimio na Mtimbwa, Manispaa ya Sumbawanga, wamepata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea yanayolenga kuongeza tija ya uzalishaji na kupunguza matumizi yasiyo sahihi ya pembejeo. Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wakulima kuelewa aina sahihi za mbolea, viwango vinavyopaswa kutumika, na muda unaofaa wa matumizi kulingana na hali ya udongo na mahitaji ya mimea.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Udhibiti Ubora wa Mbolea, Bw. Mushoborozi Christian, amesema elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika kuhakikisha wakulima wanatumia mbolea kwa usahihi ili kuongeza uzalishaji na kulinda rutuba ya udongo.

“Mafunzo haya yana lengo la kumsaidia mkulima kutumia mbolea kulingana na mahitaji halisi ya shamba lake. Tukitumia mbolea kwa usahihi, tutaongeza mavuno na kupunguza gharama zisizo za lazima,” alisema Bw. Mushoborozi.

Sambamba na mafunzo hayo, wakulima walipata fursa ya kusajiliwa katika mfumo wa ruzuku ya mbolea, hatua inayowawezesha kununua mbolea kwa bei nafuu na kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Mfumo huo pia unalenga kuboresha uwazi na usimamizi wa utoaji wa ruzuku.

Mmoja wa wakulima walionufaika na mafunzo hayo, Bw. Christopher Abel, amesema mpango huo ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa Sumbawanga, kwani utawasaidia kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji.

“Zamani tulikuwa tunatumia mbolea kwa mazoea bila kujua aina gani inafaa kwa mazao yetu. Sasa tumeelimishwa, na kwa msaada wa ruzuku, tunaweza kulima kwa ufanisi zaidi,” amesema Bw. Abel.

Mafunzo haya ni sehemu ya kampeni endelevu ya Serikali kupitia programu ya “Mali Shambani: Silaha Mbolea”, inayolenga kuwawezesha wakulima kote nchini kufahamu matumizi sahihi ya mbolea na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.



Post a Comment

Previous Post Next Post