Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Tanga imekabidhi mifuko ya Sukari 433 pamoja na madumu 48 ya mafuta ya kula vyote kiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 63 ikiwa ni utekelezaji wa Maagizo ya Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda kuwa bidhaa hizo zilizoingizwa nchini kinyume na sheria zigawanywe kwa watu wenye mahitaji.
Bidhaa hizo zimekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dr. Batilda Burian, Ijumaa tarehe 10.10.2025 huko katika Kituo cha Forodha cha Horohoro na Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Bw. Gelas Kinabo pamoja na Mkuu wa kituo cha Horohoro OSBP Bw. Shedrack Mbonea.
Mhe. Batilda amesema bidhaa hizo zitagaiwa kwa makundi mbalimbali ya wenye uhitaji katika jamii kama vile watoto yatima na wazee.
Akizungumza wakati wa Makabidhiano hayo Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dr. Batilda Burian, aliwaasa wafanyabiashara kuacha kutumia njia zisizo rasmi katika uingizaji wa bidhaa nchini ili kuepuka madhara na adhabu zinazoweza kujitokeza.
Mbali na hayo, Mhe. Batilda ametoa shukrani zake za dhati kwa TRA mkoa wa Tanga kwa namna wanavyoendelea kukusanya kodi kwa weledi huku akiwataka kuendelea kufanya hivyo kwa maslahi ya Taifa.
Naye Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa Tanga Bw. Gelas Kinabo amesema ugawaji wa bidhaa hizo ni sehemu ya mipango ya TRA  kutoa bidhaa ambazo zimengizwa nchini kinyume na sheria kwa watu wenye mahitaji katika jamii huku akiwasisitiza wafanyabiashara kufuata taratibu za kiforodha wanapoingiza mizigo nchini  kwa kuhakikisha wanatii sheria za kodi zilizopo.




