WIZARA YA NISHATI YAKAGUA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA TAASISI ZINAZOLISHA WATU ZAIDI YA 100 ILEMELA

Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia,  Nolasco Mlay pamoja na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati   wameanza ziara ya kikazi mkoani Mwanza kwa lengo la kukagua utekelezaji wa agizo la Serikali kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia Nishati Safi ya Kupikia.

Ziara hiyo imeanza kwa kukagua  shule tatu za Sekondari katika Manispaa ya Ilemela ambazo zimeanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia baada ya kunufaika na mradi wa CookFund kupitia mpango wa kimataifa wa Integrated Approach to Sustainable Clean Cooking Solution unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).

Ziara hiyo pia inalenga kufanya tathmini ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa taasisi zinazopokea ufadhili kutoka mradi wa CookFund.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Nolasco Mlay amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati  wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), ambao unalenga kuhakikisha taasisi za umma ikiwemo shule, zinatumia teknolojia salama na rafiki kwa mazingira katika upishi.

Katika kuhakikisha kuwa agizo hilo la Serikali linatekelezwa kwa mafanikio, Mlay amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa ambao bado taasisi katika maeneo yao hazijahama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi  ya kupikia kuhakikisha kuwa wanatekeleza Mkakati  wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

"Taasisi za Umma na Binafsi katika maeneo yenu kama vile Shule, Hospitali, Magereza pamoja Jeshi zinapaswa kutumia teknolojia salama na rafiki kwa mazingira katika upishi ili kuepusha athari za kiafya na kimazingira kwa nchi." Amesema Mlay

Sambamba na hilo,  Mlay amewahimiza Walimu na Wakuu wa Shule kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wanafunzi juu ya faida ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili wawe mabalozi  wa kuelimisha wengine.



Post a Comment

Previous Post Next Post