Wakulima Rukwa Waadhimisha Siku ya Mbolea Duniani Kivingine

Katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Mbolea Duniani, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) pamoja na kampuni za mbolea nchini, imeendelea na kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima. Kampeni hii inalenga kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu matumizi bora ya mbolea kwa kuzingatia kanuni nne kuu za matumizi sahihi, pamoja na umuhimu wa kupima afya ya udongo ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Utekelezaji wa kampeni hiyo umeanza katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na Rukwa, ambapo timu za wataalam zimekuwa zikifika mashambani kutoa elimu ya vitendo kuhusu namna bora ya kutumia mbolea kulingana na mahitaji halisi ya udongo na mazao.

Akizungumza na wakulima wa vijiji vya Mkoe na Ilambila vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Samson Poneja, amesema upatikanaji wa mbolea nchini umeongezeka kutoka tani 560,551 mwaka 2021/22 hadi kufikia tani 1,323,799 mwaka 2024/25. Aidha, matumizi ya mbolea yamepanda kutoka tani 363,598 hadi tani 972,074 katika kipindi hicho, hatua inayodhihirisha mafanikio ya kampeni za uhamasishaji na mpango wa ruzuku ya mbolea.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Nicholas Eliadu, ameipongeza Serikali kwa juhudi hizo, akibainisha kuwa kampeni hiyo imeongeza ari ya wakulima kutumia mbolea kwa usahihi, jambo linalochochea ongezeko la uzalishaji na kipato cha kaya za wakulima.

Mkulima wa maharage kutoka Kalambo, Benard Agustino, amesema kupitia ruzuku ya mbolea ameongeza mavuno kutoka magunia 6–9 hadi 15–20 kwa msimu. Amesisitiza kuwa matumizi ya mbolea sahihi kwa kuzingatia ushauri wa wataalam ni hatua muhimu ya kuinua uzalishaji na kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wakulima.

Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani hufanyika kila mwaka Oktoba 13 yakiwa na lengo la kuelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea, kuongeza uzalishaji wa mazao, na kuchochea maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo nchini.



Post a Comment

Previous Post Next Post