#Yasherehekea na wakulima shambani
Mwandishi Wetu,
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Joel Laurent amewasihi wakulima kuhuisha taarifa zao za mashamba katika mfumo wa usajili wa wakulima ili kuwawezesha kupata mbolea kulingana na uhitaji wao kwa kuwa wakulima hao wanakuwa shambani kwa mwaka mzima katika maeneo wanayolima.
Ametoa wito huo kwa wakulima wa Kijiji cha Ujindile Kata ya Igosi mkoani Njombe ambapo hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani kwa mwaka 2025 yamefanyika.
Ameeleza pia kuwa lengo kuu la kuwepo ni kubadilishana uzoefu kati ya wakulima, wataalamu na wazalishaji na waingizaji wa mbolea ili kuongeza tija katika shughuli za kilimo.
“Kuna maeneo maalum kama Mamlaka tumeona ni vyema kuyatazama upya.
Tumeongeza idadi ya mifuko ya mbolea kwenye eneo la viazi, na tumeanza kuona vijana wakijitokeza zaidi kutokana na tija wanayoiona kwenye kilimo.
Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima jirani na mashamba yao,” amesema Laurent.
Aidha, amewasihi wakulima kupima afya ya udongo ili waweze kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na aina ya zao wanalolima.
“Tunataka wakulima waendelee kupima afya ya udongo, kutumia mbolea kwa usahihi na kulima kwa tija.” amesema Laurent.
Kwa upande wake, Heri Chengula mkulima wa parachichi kutoka kijiji cha Ujindile, ameishukuru Serikali kupitia TFRA kwa kuendelea kuwezesha wakulima kupata mbolea za ruzuku kwa urahisi zaidi.
“Mbolea za ruzuku zimetupa unafuu mkubwa sana na uzalishaji wa mazao ya mahindi umeongezeka kutoka kuvuna gunia moja hadi 15 baada ya kuanza kutumia mbolea za viwandani,” amesema Chengula.
“Tunaendelea kujifunza kuhusu namna sahihi ya kutumia mbolea kwenye mazao mbalimbali, na tunashukuru kwa juhudi za TFRA kutusogezea huduma hizi karibu,” ameongeza Mwalongo.
Kwa mwaka huu 2025 Mamlaka imeadhimisha Siku ya Mbolea Duniani kwa kupeana uzoefu na wakulima na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea katika mikoa ya Njombe, Mbeya, Tanga, Rukwa na Manyara, Kagera na elimu hii inaendelea nchi nzima ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya Mali shambani, Silaha Mbolea.





