Mwandishi Wetu,
Wakulima wa mpunga kutoka vijiji vya Mkwajuni na Kasekese, wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, wameeleza kufurahishwa na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea wanayopewa na wataalamu wa kilimo kupitia kampeni ya uhamasishaji inayoendeshwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Bukwimba Makumucha, mmoja wa wakulima wa mpunga kijijini Mkwajuni, amesema elimu hiyo imemsaidia kuongeza uzalishaji wake kwa kiwango kikubwa, huku akipongeza juhudi za serikali kuhakikisha mbolea za ruzuku zinapatikana kwa wakati.
“Kabla ya mfumo wa ruzuku nilikuwa napata gunia kati ya 8 hadi 10 kwa ekari, lakini sasa napata kati ya gunia 20 hadi 30 za mpunga. Mbolea za ruzuku zimenisaidia sana, maana zamani mfuko mmoja wa mbolea tulikuwa tunanunua kwa shilingi 150,000, lakini sasa tunapata kwa shilingi 75,000 tu. Huu ni msaada mkubwa kwa mkulima,” alisema Makumucha.
Naye Maulid Macha, mkulima kijijini Kasekese, amesema elimu ya matumizi sahihi ya mbolea imebadilisha kabisa namna wanavyofanya kilimo, hasa kwa vijana wanaoanza kujikita katika sekta hiyo.
“Tunamshukuru sana Waziri wa Kilimo na TFRA kwa kutuletea wataalamu wanaotufundisha kutumia mbolea kwa usahihi. Sasa tunafanya kilimo cha kisasa zaidi, na tumeona matokeo yake. Mimi mwenyewe napata kati ya gunia 25 hadi 30 za mahindi kwa ekari, tofauti na zamani,” alisema Macha.
Ameongeza kuwa mfumo wa ruzuku ya mbolea na mbegu umeleta matumaini mapya kwa vijana wa vijijini, akihimiza wenzake kutambua kuwa kilimo ni biashara yenye tija.
“Nawaambia vijana wenzangu tuache dhana kwamba kilimo ni kazi ya wazee. Sasa hivi kilimo kinalipa, na serikali imerahisisha mambo kupitia ruzuku. Ni fursa ya kizazi chetu kuamka,” amesisitiza.
Kupitia kampeni ya “Mali Shambani: Silaha Mbolea,” wizara ya kilimo inaendelea kutoa elimu kwa wakulima nchini kote kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, usajili wa wakulima kwenye mfumo wa ruzuku, na umuhimu wa upimaji wa afya ya udongo ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuinua kipato cha mkulima.