Na Mashaka Mgeta, MUHEZA
KATIKATI ya misitu ya miti ya kupanda, mashamba ya mazao na viungo wilayani Muheza Mkoa wa Tanga, kuna ‘vijito’ vinavyoingiza maji Mto Zigi katika wilaya za Tanga, Mkinga, Pangani na Muheza yenyewe.
Lakini, kwenye maeneo kadhaa yenye ‘vijito’ hivyo, wameibuka watu kiholela wanaochimba dhahabu, hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira.
Vicent Ernest, kwa niaba ya wakulima wenye mashamba kwenye maeneo yanayopitiwa na Mto Zigi na vyanzo vingine vya maji, anasema wavamizi hususani vijana, wanafika hasa nyakati za usiku na kuchimba dhahabu kiholela hivyo uharibifu wa mazingira.
Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TangaUWASA) na wadau wengine, imechukua hatua kadhaa za kuhifadhi mazingira ya maeneo hayo, ikiwemo uanzishwaji na uendelezaji wa Umoja wa Wakulima Wahifadhi wa Mazingira Kihukwi Zigi (UWAMAKIZI).
UWAMAKIZI iliyoanzishwa mwaka 2013 ikiwa na wanachama 473, inajihusisha na hifadhi ya mazingira hayo na sasa idadi yao imefikia 1,825.
Mwenyekiti wa UWAMAKIZI, Rajab Mbarouk, anasema pamoja na jitihada hizo, suala la uvamizi wa wachimbaji holela wa dhahabu limebaki kuwa changamoto inayohitaji suluhu ya kudumu.
Hoja hiyo inatolewa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TangaUWASA, Dkt Fungo Ali Fungo amesema, uvamizi huo unaathiri jitihada za Mamlaka hiyo kuhifadhi mazingira ya Mto Zigi, ambapo kwa kipindi cha 2013 hadi 2025 imetumia Shilingi milioni 820.
Oktoba 9, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amepiga marufuku uchimbaji holela huo, alipotembelea maeneo hayo, akianzia kwenye ‘kijito’ cha Zisa ambacho kama ilivyo kwa ‘vijito’ vya Nunguhi, Kiwea na Kihuhwe, maji yake yanaingia Mto Zigi.
Mhe Balozi Dkt Batilda, anasema uhifadhi utapewa umuhimu kupitia elimu kwa jamii na mbinu rafiki za kupata suluhu ya kudumu.
Februari 27, 2025, Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, akiwa ziarani Mkoa wa Tanga, aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji Mkinga – Horohoro wenye thamani ya Shilingi bil 35.4, na kuagiza utunzaji vyanzo vya maji vya Mto Zigi.