MBOLEA YA RUZUKU YAONGEZA UZALISHAJI WA VIAZI RUNGWE.

Wakulima wa Wilaya ya Rungwe wameendelea kunufaika na mpango wa ruzuku ya mbolea unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka  ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania(TFRA) hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao, hususan zao la viazi. 

Obadia Mwansasu, mkulima wa viazi kutoka Rungwe, amesema anaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kwa kuanzisha mpango wa ruzuku ya mbolea, ambao umemuwezesha kufanya kilimo chenye tija tofauti na awali ambapo alikuwa analima kwa mazoea.

“Mpango wa ruzuku umenisaidia sana, zamani katika ekari moja nilikuwa napata gunia 30 pekee, lakini sasa kwa kutumia mbolea kwa usahihi napata gunia 140 za viazi. Hii imeniongezea kipato na kuinua maisha yangu,” amesema Mwansasu.

Kwa upande wake, Bariki Mwansasu amesema hapo awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za mbolea, lakini kupitia ruzuku wameweza kuzalisha kwa tija zaidi. Ameongeza kuwa vijana wengi sasa wameanza kujihusisha na kilimo kutokana na urahisi wa upatikanaji wa pembejeo za ruzuku.

“Awali tulikuwa tunalima kwa mazoea, lakini sasa tunashukuru serikali yetu. Nimetambua kweli ukitaka mali utaipata shambani, na silaha ni mbolea,” amesema Bariki kwa furaha.

Akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Mazao Wizara ya Kilimo Bw. Samson Poneja, amewataka wakulima kote nchini kuendelea kujisajili kwenye mpango wa ruzuku na kupima afya ya udongo ili kutumia mbolea sahihi kulingana na mahitaji ya udongo. Amehimiza matumizi ya mbolea kwa kufuata ushauri wa wataalam ili kuongeza tija na kuboresha uzalishaji.



Post a Comment

Previous Post Next Post