NISHATI SAFI YA KUPIKIA SULUHU KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI




Watanzania wameendelea kuhamasishwa kutumia nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Wito huo umetolewa leo Agosti 18, 2025 Mkoani Rukwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Florian Haule wakati wa ugawaji wa mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Rukwa unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akiwa ameambatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Stephen Mwakifwamba, Haule amewataka pia maafisa pamoja na askari wa jeshi hilo kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa jamii inayowazunguka.

“Ni ukweli usiopingika kwamba Jeshi la Magereza hapo nyuma walikuwa ni wakala wakubwa wa uharibifu wa mazingira kwa kutumia kuni na mkaa kwa ajili ya kuandaa chakula cha wafungwa magerezani, hali iliyopelekea uharibifu wa mazingira hasa uoto wa asili. Lakini kwa sasa magereza yote yanatumia nishati safi ya kupikia.

Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanakwenda kuokoa mazingira yetu na hivyo kupunguza madhara ya kiuchumi pamoja na kijamii ambayo yanatokana na mabadiliko ya tabia nchi. Niendelee kuwahamasisha mkawe mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia ili tuendelee kulinda mazingira yetu,” amesema Haule.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Vendeline Tesha amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha magereza yote katika Mkoa huo kufungwa mifumo ya nishati safi ya kupikia na kuwezesha pia askari wa jeshi hilo kupata majiko ya gesi na kuongeza kuwa kitendo hicho kitaenda kuongeza morali ya kazi kwa watumishi hao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili maono ya Mhe. Rais pamoja na malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umebainisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia yanafikiwa.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Afisa kutoka REA, Mhandisi Francis Manyama amesema kuwa kwa Mkoa wa Rukwa, jumla ya mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 297 yamepangwa kugaiwa kwa watumishi wa jeshi la magereza katika Mkoa wa Rukwa.

Septemba 13, 2024, REA iliingia makubaliano ya utekelezwaji wa mradi wenye gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 35 na Jeshi la Magereza wa kuwezesha kutoa ruzuku kwa ajili ya kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa magereza yote ya Tanzania Bara.

















Post a Comment

Previous Post Next Post