
Watanzania na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasishwa kushirikiana na Serikali ili kufanikisha malengo yaliyowekwa ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umelenga kufikia mwaka 2034 zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Wito huo umetolewa leo Agosti 20, 2025 Jijini Mbeya na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Florian Haule wakati wa ugawaji wa mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mbeya unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akiwa ameambatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Stephen Mwakifwamba, Haule amewataka pia maafisa pamoja na askari kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuwa mabalozi na kuwahamasisha jamii inayowazunguka kutumia nishati safi ya kupikia.
“Tunapenda kuendelea kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo imelenga kuendelea kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kutunza mazingira.
Sisi kama Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tunaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kutekeleza maono ya Mhe. Rais pamoja na Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia. Serikali pekee haiwezi kufanikisha malengo yaliyoainishwa katika mkakati huo, hivyo tuendelee kuwahamasisha mkawe mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa ndugu, jamaa na jamii inayowazunguka ili kwa pamoja tufanikishe lengo la Watanzania asilimia 80 kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” amesema Haule.
Kwa upande wake Mwppakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa REA iliingia makubaliano na Jeshi la Magereza kutekeleza mradi wa kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza yote nchini.
Amesema kuwa mradi huo wenye gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 35 ambapo REA, imetoa zaidi ya shiliningi Bilioni 26.5 kwa ajili ya kufungwa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza yote nchini pamoja na kugawa mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa watumishi wote wa jeshi hilo ni miongoni mwa mikakati inayotekelezwa na REA kuhamasiha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Miradi kutoka REA, Mhandisi Francis Manyama amesema kuwa kwa Mkoa wa Mbeya, jumla ya mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 895 yamepangwa kugaiwa kwa watumishi wa jeshi la magereza katika Mkoa huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Raymond Mwampashi kwa niaba ya watumishi wa jeshi hilo kwa Mkoa wa Mbeya ametoa pongezi zake kwa Serikali kwa kuwapatia watumishi majiko hayo ya gesi na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi kwa wengine na kuwahamasisha kutumia nishati safi ya kupikia.








