TFRA Yatoa Elimu ya Mbolea na Kusajili Wakulima Katika Maonesho ya NaneNane Lindi

 Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Kilimo ya NaneNane yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi, kwa lengo la kutoa elimu na huduma mbalimbali kwa wadau wa kilimo.

Kupitia banda lake, TFRA imejikita katika kuelimisha wakulima, wafanyabiashara wa pembejeo na wananchi kwa ujumla kuhusu majukumu yake katika kusimamia mnyororo mzima wa thamani wa mbolea kuanzia uingizaji, uzalishaji, usambazaji hadi kwa mtumiaji wa mwisho.

Akizungumza katika banda hilo, Meneja Kanda Mashariki, Daniel Maarifa, alisema kuwa Mamlaka inatoa elimu ya kina kuhusu umuhimu wa kupima afya ya udongo kabla ya matumizi ya mbolea ili kuhakikisha matumizi sahihi ya mbolea kwa tija ya kilimo.

 “Kupima afya ya udongo ni hatua ya msingi inayomsaidia mkulima kujua aina na kiwango sahihi cha mbolea anachopaswa kutumia kwa mazao yake,” alisema.

Aidha, TFRA inaendelea na zoezi la usajili wa wakulima ambao bado hawajapata namba ya utambuzi wa wakulima, ambayo ni muhimu ili waweze kunufaika na mpango wa ruzuku ya mbolea unaoratibiwa na Serikali kupitia mfumo wa kidigitali wa TFRA.

Wakulima wengi wanaotembelea banda hilo wamepongeza juhudi za TFRA kwa kutoa huduma muhimu na elimu inayolenga kuongeza ufanisi katika kilimo na kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

Maonesho ya NaneNane ni jukwaa muhimu kwa taasisi kama TFRA kukutana moja kwa moja na wadau wa kilimo na kutoa elimu itakayosaidia kuleta mapinduzi ya kilimo nchini Tanzania.



Post a Comment

Previous Post Next Post