Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetumia Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya J.K. Nyerere mkoani Morogoro kuwahudumia wakulima kwa kutatua changamoto mbalimbali, ikiwemo elimu duni juu ya matumizi sahihi ya mbolea, matumizi ya vifaa kinga, upatikanaji wa leseni kwa wauzaji wa pembejeo, pamoja na kusaidia wakulima waliopoteza kumbukumbu za namba zao za ruzuku.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Raymond Konga, alisema kuwa taasisi hiyo imepokea idadi kubwa ya wakulima waliokuja kwa ajili ya kupata msaada wa kitaalamu na kwamba kila changamoto imefanyiwa kazi kwa wakati.
“Wakulima wamekuwa wakifika na kueleza changamoto zao, na sisi kama TFRA tumekuwa tukiwahudumia kwa kuwapa elimu, ushauri na msaada wa moja kwa moja. Tunahakikisha kila anayefika anapata suluhisho,” alisema Konga.
Baadhi ya wakulima waliopata huduma kutoka TFRA wameeleza kuridhishwa kwao na huduma walizopokea. Kilala Mayaya, mkulima kutoka Wilaya ya Malinyi, alisema kuwa elimu aliyopewa kuhusu matumizi ya vifaa kinga imemfungua macho na sasa ataweza kulinda afya yake anapokuwa shambani.
“Sikuwa natumia vifaa kinga, lakini sasa nimeelewa umuhimu wake. Nitashiriki elimu hii na wakulima wengine,” alisema Mayaya.
Kwa upande mwingine, Michael Mbilinyi, mfanyabiashara wa pembejeo, alieleza kufurahishwa baada ya kupata msaada wa kusajili biashara yake na kupewa mafunzo ya jinsi ya kupata leseni halali ya kuuza mbolea.

