JAJI MKUU AFUNGUA MLANGO MABORESHO YA SHERIA, SERA



NA MWANDISHI WETU, DODOMA


JAJI Mkuu wa Tanzania,George Masaju amekaribisha maoni ya watanzania kuboresha Sheria na Sera mbalimbali ili kuchochea utawala wa sheria,ukuzaji wa demokrasia na Ustawi wa wananchi.


Akizungumza wakati akifungua mjadala wa kitaifa ya kujadili maboresho ya sheria na sera nchini, ulioandaliwa na Mtandao wa watetezi wa.haki za binaadamu nchini(THRDC) na Vyama vya Wanasheria,Jijini Dodoma Augost 10,2025, Jaji Masaju alisema milango ya majadiliano ipo wazi lakini muhimu mabadiliko yanayoombwa yawe yanazimgatia maslahi ya umma na kulinda Katiba ya Nchi.


"Serikali hatujafunga mipango,leteni maboresho ya sheria lakini pia lazima yatokane na matakwa ya wananchi sio mashinikizo kutoka nje na pia mje na hoja na sababu za kutaka maboresho hayo"alisema


Alisema ni muhimu wanasheria na watanzania kwa ujumla kutambua haiwezekani kuwa na mabadiliko kwa kuiga wengine kwani watanzania wana historia yao,mila na taratibu na kuiga kila kitu nchi kunaweza kubomoa nchi.


"Sheria zinakwenda hatua kwa hatua hatuwezi kukimbilia kila kitu na tunataka sheria na sera zitakazoleta ongezeko la thamani na ustawi wa wananchi"alisema


Hata hivyo, Masaju alipongeza THRDC kwa kuandaa kongamano hilo ambalo linaleta majadiliano ya pamoja ya maboresho ya sheria na Sera kwa kukaa mezani.


"Mimi nawapongeza sana THRDC kupitia mratibu wenu Ole Ngurumwa  nimewafatilia naona nyie mnahoja na tutaendelea kushirikiana kuboresha sheria na Sera"alisema


Alisema vyama vingine vya kitaaluma na mashirika mengine pia wanaweza kuleta hoja na kujadiliwa kwa pamoja kwa sababi Tanzania sio ya kundi fulani fulani bali ni ya watanzania wote wenye nia njema ya kuchochea ustawi wa wananchi.


Awali,Mwenyekiti wa baraza la Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini(NaCoNGO) Mwantumu Mahiza alisema serikali inatambua kazi nzuri za Asasi za kiraia nchini.



Mahiza alisema changamoto zilizopo zinaendelea kufanyiwa kazi na hatua kubwa imepigwa katika kutatua changamoto za Asasi za Kiraia nchini tofauti na miaka ya nyuma.


Mratibu wa Kitaifa wa THRDC,Wakili Onesmo Ole Ngurumwa alisema THRDC kwa kushirikiana na vyama vya Mawakili inaona kuna haja ya kuwepo maboresho ya sheria kadhaa ili kuchochea ukuaji ukuaji wa demokrasia,kutominywa utendaji kazi wa Asazi za kiraia,kuchochea ustawi wa wananchi na ulinzi wa haki za binaadamu.


Ole Ngurumwa alisema kupitia tafiti na chambuzi mbalimbali zilizofanywa ukiwepo uliofanywa kutazama hali ya mfumo wa utetezi wa haki za binaadamu nchini na  pengo la uwezo na mahitaji ya Asasi za kiraia nchini uliofanywa na Wakili Clarence Kipobota  unaonesha mahitaji ya maboresho ya sheria na sera.


Katibu wa chama cha Mwakili wa Afrika Mashariki(EALS) John Seka na Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji, Elimo Massawe kwa pamoja walihimiza ushirikiano wa wadau wote katika kulinda na kutetea haki za binadaamu nchini kwa kuzingatia sheria.


Akifunga kongamano hilo,Kamishna wa tume ya mabadiliko ya sheria,Dk Idd Mandi alisema tume yake ipo tayari kupokea maboresho ya sheria na sera wakati wowote kwa kuzingatia maslahi ya Umma.


Alisema baada ya kuzinduliwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,Tume ya mabadiliko ya sheria inakaribisha.maoni na wadau ya kutungwa sheria na sera za kuwezesha Dira ya Taifa kufanya kazi na kuleta matokeo chanya.


Kongamano hilo liliandaliwa na Mtandao wa  Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), Umoja wa Wanasheria wa Afrika (PALU), na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kwa udhamini wa  Umoja wa Ulaya.


Post a Comment

Previous Post Next Post