KRETA YA NGORONGORO YAMVUTIA MEYA WA JIJI LA DALLAS MAREKANI, AAHIDI KUREJEA NA FAMILIA YAKE

 Na Mustapha Seifdine, Ngorongoro Kreta.

Eneo la hifadhi ya Ngorongoro limeendelea kuwa kimbilio la wageni mashuhuri duniani ambapo siku ya leo,  Meya wa Jiji la Dallas nchini Marekani, Mhe. Eric Johnson kwa mara ya kwanza ameshuhudia upekee wa vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo.

Meya huyo aliyefuatana  na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza amepokelewa na  Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Abdul-Razaq Badru na kuwaeleza kuwa eneo la hifadhi ya Ngorongoro lina utajiri wa vivutio vya utalii ikiwepo Kreta ya Ngorongoro, Wanyama wakubwa watano "Big Five",  bonde la Olduvai lenye gunduzi mbalimbali za Zamadam, tambarare za Ndutu ambazo ni mazalia ya Nyumbu, mchanga unaohama, Nyayo za Laetoli zenye umri wa miaka Mil 3.7 iliyopita na vivutio vingine vingi.

Kamishna Badru alieleza kuwa Ngorongoro si tu kivutio cha utalii bali ni  ni somo la uhai linaloishi. 

“Hapa ndipo unaweza kuwaona faru weusi katika mazingira yao ya asili, jambo ambalo ni nadra duniani. Na juhudi zetu za kulinda viumbe hawa walio hatarini kutoweka zinaendelea ili kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo,” alisisitiza.

Kwa upande wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Huduma za Utalii na Masoko, Mariam Kobelo, alieleza kuwa hifadhi ya Ngorongoro ni eneo lenye hadhi tatu za  kimataifa zinazotambuliwa na UNESCO ambazo ni Hifadhi ya Binadamu na Baiolojia, Urithi wa Dunia Mchanganyiko unaojumuisha maliasili na utajiri wa kiutamaduni unaoshikilia historia ya mwanadamu na hadhi ya tatu ni eneo lenye hadhi ya utalii wa miamba (Ngorongoro Lengai Global Geopark).

Akielezea furaha yake baada ya kufika hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni kivutio namba moja cha utalii Afrika Meya Eric Johnson amesema kuwa; “Huu ni uzuri usioelezeka, ni mara yangu ya kwanza kufika Afrika, na hapa Ngorongoro nimeshuhudia wanyama wa kila aina, mandhari ya kuvutia, na mfumo wa ikolojia ambao ni wa kipekee duniani. Naahidi kurudi tena na familia yangu.”



Post a Comment

Previous Post Next Post