Mwandishi Wetu,
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amekagua mradi wa maji wa miji 28 mjini Karagwe na kumtaka mkandarasi kampuni ya Blasb Associate & Co kutatua changamoto za vibarua ikiwemo kutoa mikataba.
Waziri Aweso ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa vibarua kuhusu kutokuwa na mikataba ya kazi.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha upatikanaji wa fedha kwa wakati jambo ambalo limewezesha malipo ya mkandarasi kwa wakati hivyo hana kisingizio.
Amesema serikali inatambua umuhimu wa huduma ya majisafi kwa wananchi lakini bado inazingatia maslahi na haki ya wafanyakazi.
Umuhimu huo ndio umekuwa ukiifanya serikali izingatie kutoa kandarasi kwa wazawa wakiwemo kampuni ya Blasb Associate & Co ili wafaidi matunda ya uwekezaji wa serikali.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso amemteua Mhandisi Magreth Nyange kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka na atapangiwa kituo cha kazi.
Amechukua hatua hiyo kufuatia usimamizi mzuri wa mradi huo ambao hadi sasa umefika ailimia 64 ya utekekezaji ambapo Mhandisi Magreth ameonesha uwezo mkubwa wa kufuatilia, kusimamia na kushauri namna bora ya kufanikisha utekekezaji wa mradi.
Kwa sasa Mhandisi Magreth ni Msimamizi wa Kanda ya Karagwe ambako mradi huo unatekelezwa. Kanda hiyo ipo chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba.