Aweso aagiza ujenzi chanzo cha maji Rujewa kukamilika Septemba 2025

Mwandishi Wetu,

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametaka ujenzi wa chanzo cha maji cha Mradi wa maji miji 28 eneo la Rujewa,  Mbeya kazi ikamilike Septemba 2025.

Aidha, ameagiza utekelezaji wa mradi huo ufanyike usiku na mchana ili kufidia mapungufu ya muda. 

Amesema hayo  baada ya kukagua mradi huo unaotarajiwa kuongeza huduma ya maji katika wilaya ya Mbarali kutoka siku mbili kwa siku saba hadi kufika  asilimia 95 ambayo itawezesha huduma ya maji kwa siku saba za wiki. 

Aweso amesema haridhishwi na kasi ya utekelezaji wa mradi ambao sasa umefika asilimia 35. Amesisitiza na kumuagiza Mkuu wa Wilaya  hiyo  kusimamia kwa karibu kuhakikisha mkandarasi anaongeza nguvu kazi kwa kuwapa  vijana wazawa  kipaumbele. 

Mhe. Aweso amesema agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mradi unakamilika na kwamba fedha zote za utekekezaji wa mradi zipo. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri  ambaye ameambatana na Waziri Aweso katika kazi   hiyo amesisitiza na kumtaka mkandarasi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba na kwamba ofisi yake haitasita kuchukua hatua iwapo maagizo yaliyotolewa na hayatatekelezwa



Post a Comment

Previous Post Next Post