NA MWANDISHI WETU,
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson, amemshukuru na kumpa pongezi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA) Yusuph Mwenda kwa kazi nzuri anayofanya ya kukusanya Kodi nchini.
Pia ametoa wito kwa wabunge kama wawakilishi wa wananchi kuhakikisha wanakuwa mfano bora katika kulipa kodi ili kusaidia nchi kupiga hatua zaidi katika ukusanyaji mapato na nyanja nyingine.
Tulia ametoa pongezi hizo, jana katika kikao cha 12 cha Bunge mkoani Dodoma ambapo, Kamishna Mwenda alikuwa mgeni mwalikwa.
"Kwa yale tunayosema kila siku kuhusu mapato ya ndani na makusanyo watu walipe kodi, basi kipekee kabisa nichukue fursa hii, kumshukuru na kumpongeza sana, Kamishna Mkuu wa TRA kwa kazi nzuri anayofanya.
Tunaamini kwa hatua ambazo zinaendelea kupigwa basi, makusanyo yataendelea kuongezeka," amesema. Pia Tulia amemtakia kila la kheri, Kamishna Mwenda kuhakikisha mapato yanaendelea kuongezeka kila siku.