Mwandishi Wetu,
Juhudi za Serikali kupitia ushirikiano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bodi ya Pamba na Mradi wa Building a Better Tomorrow – Youth Initiative for Agribusiness (BBT) zimesaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la pamba kwa wakulima wa Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, na kubadili mtazamo wao kuhusu matumizi ya mbolea.
Awali, wakulima wengi wa wilaya hiyo walikuwa na imani potofu kuwa mbolea inaharibu ardhi, jambo lililosababisha wao kushindwa kuzalisha kwa tija na hivyo kuchelewa kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza tarehe 13 Mei 2025, Afisa Ugani chini ya Mradi wa BBT, Juni Ezekia Bitana, alieleza kuwa kupitia juhudi za pamoja baina ya wadau hao, wakulima walifundishwa Kanuni 10 Bora za Kilimo cha Pamba, ikiwa ni pamoja na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Bitana alifafanua kuwa halmashauri ya Kishapu ilipokea kifaa cha kupima afya ya udongo kilichotumika kupima mashamba ya wakulima wa mfano.
Bitana ameeleza kuwa, matokeo ya vipimo hivyo yalisaidia kutoa elimu sahihi kwa wakulima kuhusu aina na kiwango cha mbolea kinachotakiwa, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa na matumizi sahihi ya pembejeo hiyo muhimu.
“Licha ya changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, wakulima wameweza kuzalisha vizuri msimu huu na wameonyesha dhamira ya kuendeleza kilimo bora,” alisema Bitana.
Wakulima wa pamba wa wilaya ya Kishapu walioshiriki katika mafunzo hayo wameeleza kuwa, awali walikuwa wakilima bila kutumia mbolea kwa hofu ya kuharibu udongo na kubaini kuwa si kweli.
Ameeleza kuwa, baada ya kupatiwa elimu, wakulima hao wameanza kutumia mbolea na kuahidi kuwa mabalozi wa kuelimisha wakulima wengine kuhusu umuhimu wa mbolea katika kuongeza uzalishaji.
Walisema kuwa msimu huu pamba ilistawi vizuri, ambapo kila tawi lilikuwa na wastani wa vitumba 90 hali iliyowafanya kuwa na matarajio ya kuvuna maradufu ya walivyokuwa wakivuna awali, ingawa ukame uliyojitokeza mwishoni mwa msimu ulisababisha kupukutika kwa matunda na kueleza hata hivyo wanamatarajio ya kuvuna zaidi kuliko misimu ya nyuma.





