Wadau wa mbolea watakiwa kutoa huduma bora kwa wakulima

Mwandishi Wetu,

Washiriki wa mafunzo ya biashara ya mbolea wametakiwa kusikiliza na kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo ili waweze kutoa huduma bora kwa wakulima wanaowahudumia mara baada ya mafunzo hayo.

Wito huo umetolewa na Afisa Kilimo wa Manispaa ya Morogoro, Shaban Charles alipokuwa akifungua mafunzo ya mbolea yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) tarehe 12 Mei 2025. 

 Mafunzo hayo ya siku mbili (12–13 Mei 2025) yamefanyika katika Ukumbi wa Amabilis Center (Mgolole Sister), mkoani Morogoro Morogoro  kwa ushirikiano baina ya TFRA na wataalam kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo -MATI Ilonga.

Akieleza umuhimu wa mafunzo hayo Mratibu kutoka TFRA,  Azizi Mtambo amesema, yamekusudia kuwajengea uwezo wadau wa tasnia ya mbolea kuhusu matumizi sahihi, salama, na yenye tija ya mbolea, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka wa kuimarisha huduma kwa wakulima kupitia elimu kwa wasambazaji na wauzaji wa pembejeo.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na washiriki 248 kutoka mkoa huo na mikoa mingine kama shinyanga, Dar es Salaam, Geita na Rukwa ikihusisha wafanyabiashara wa mbolea, wamiliki wa maduka ya pembejeo, wanafunzi wa vyuo, na wadau wengine ambao hawakuwahi kupata mafunzo kama hayo hapo nyuma. 

Katika mafunzo hayo Mada ziliwasilishwa ikiwa ni  pamoja na; kuwawezesha wadau kufahamu majukumu na huduma zinazotolewa na TFRA, aina za mbolea na visaidizi vyake, Virutubisho vilivyopo kwenye mbolea na kazi zake, Dalili za upungufu wa virutubisho katika mimea.

Lakini pia washiriki walifundishwa juu ya ruzuku ya mbolea na namna ya kuwa wafanyabiashara wa mbolea ya ruzuku kwa kutumia mfumo wa kidigitali wa pembejeo za kilimo na nyingine nyingi.

Mtambo ameeleza kuwa, Kupitia mafunzo hayo, Mamlaka inalenga kuhakikisha kuwa kila mdau wa mbolea nchini anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, huku akichangia ipasavyo katika kuongeza tija na ustawi wa sekta ya kilimo nchini.



Post a Comment

Previous Post Next Post