Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kupitia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini - Mbeya, imewapatia wakulima wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, umuhimu wa kupima afya ya udongo, na kuhamasisha usajili wao katika mfumo wa ruzuku ya pembejeo ili kunufaika na mbolea na mbegu zinazotolewa na Serikali.
Huduma hizi zilitolewa kupitia ushiriki wa TFRA katika Maonesho ya Wakulima Festival, tukio maalum la kilimo lililoratibiwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Taasisi ya Dynamic Agriculture Program.
Akizungumza katika banda la TFRA, Bw. Nkundwe Mwambuga, Mwakilishi wa Ruzuku wa Mkoa wa Mbeya, alisema kuwa katika siku tatu za kwanza za maonesho haya ya siku sita (25–30 Aprili, 2025), wakulima 11 wamehuisha taarifa zao, wakulima 30 wamesajiliwa kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea, na zaidi ya wakulima 200 wamepatiwa huduma na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Kwa upande wake, Bw. Fadhili Alisoni, Mkurugenzi Mtendaji wa Dynamic Agriculture Program, alieleza kuwa maonesho haya yameandaliwa ili kuwapa wakulima wa vijijini nafasi ya kujifunza mbinu bora za kilimo kwa kuwa wengi wao hawawezi kufika kwenye maonesho ya kitaifa.
Alibainisha kuwa, wakulima wengi wanategemea kilimo kwa asilimia kubwa lakini wanakosa maarifa ya kitaalamu, hali inayosababisha mavuno duni licha ya juhudi zao.
Bw. Fadhili aliongeza kuwa programu hii ya elimu ya kilimo cha kisasa ni sehemu ya maono mapya ya kampuni yao, ikiwa na lengo la kufikia wilaya zote tisa za Mkoa wa Mbeya na kuchangia kuinua uchumi wa wakulima kupitia teknolojia na maarifa ya kisasa.



