Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inaendelea na zoezi la uhakiki wa taarifa za wakulima wa zao la tumbaku, kwa lengo la kufanya malipo kwa wanufaika wa mbolea za ruzuku kuanzia msimu wa kilimo 2023/2024.
Akizungumza katika ukumbi wa Benki ya CRDB wilayani Chunya tarehe 9 Aprili, 2025, Mratibu wa kikosi kazi cha uhakiki huo kutoka TFRA, Bw. Gerold Nganilevanu, amesema zoezi hilo linaendelea vizuri na linatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 20 Aprili, 2025, hatua itakayowezesha wakulima kuanza kulipwa madai yao.
Bw. Nganilevanu ameongeza kuwa, kwa sasa uhakiki huo unafanyika sambamba katika vituo vitatu ambavyo ni Chama Kikuu cha Ushirika cha Chunya (CHUTCU LTD), Mirambo na Chama Kikuu cha Ushirika WETCO cha Tabora.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tumbaku Chunya (CHUTCU LTD), Bw. Daniel Mpigasupi amesema kuwa, vyama vya ushirika 24 kutoka Wilaya hiyo vinatarajiwa kufidiwa ruzuku kwa mifuko isiyozidi 152,026 ya mbolea ya tumbaku, na kwamba vyama tisa kutoka Mkoa wa Songwe vinatarajiwa kuhakikiwa siku ya tarehe 10 Aprili 2025.
Naye Mwenyekiti wa AMCOS ya Bitimanyanga, Bw. Mawazo Mamboleo, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika, Bw. Sebastian Mogellah, ameipongeza TFRA kwa kuratibu zoezi hilo kwa ufanisi, kwani linajibu maswali mengi ya wakulima waliokuwa wakisubiri kwa hamu kunufaika na ruzuku iliyotolewa na serikali kwa ajili ya kuwanufaisha moja kwa moja.
Ameongeza kuwa, tangu kuanza kwa ruzuku hiyo, wakulima wa tumbaku wamekuwa na ari kubwa ya kufanya kazi, na kwamba mavuno kwa wanachama wake yameongezeka kutoka tani milioni 6 hadi kufikia tani milioni 27 msimu huu.





