TFRA Kanda ya Kaskazini Yatoa Mafunzo ya Matumizi Sahihi ya Mbolea kwa Wadau Jijini Arusha

Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kupitia Kanda ya Kaskazini, imeendesha mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wadau wa tasnia hiyo tarehe 9 na 10 Aprili 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Cedha, jijini Arusha.

Mafunzo hayo yamewakutanisha jumla ya washiriki 89, wakiwemo wafanyabiashara wa mbolea, wamiliki wa maduka ya pembejeo na wadau wengine wa tasnia ya mbolea ambao hawajawahi kupata mafunzo ya awali.

Wataalamu kutoka TFRA waliwasilisha mada mbalimbali zenye lengo la kuwajengea uelewa washiriki kuhusu matumizi sahihi  na salama ya mbolea, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Mamlaka kuongeza tija ya kilimo nchini. 

Baadhi ya mada zilizofundishwa ni pamoja na: Majukumu na huduma zinazotolewa na TFRA, Mbolea na visaidizi vyake,

Virutubisho vya mbolea na kazi zake, Dalili za upungufu wa virutubisho katika mimea.

Mada nyingine ni; kujua afya ya udongo na umuhimu wa kupima afya ya udongo, Sifa na umuhimu wa ghala bora la kuhifadhia mbolea,

Sifa za kifungashio bora cha mbolea na taarifa muhimu zinazopaswa kuwepo, Faida za utunzaji wa  kumbukumbu kwa wafanyabiashara, Changamoto na makosa yanayojitokeza miongoni mwa wafanyabiashara wa mbolea Kanda ya Kaskazini, Namna ya kupata kibali cha biashara ya mbolea kupitia Mfumo wa Kidigitali wa FIS na mwisho waamejifunza kuhusu  Sheria ya Mbolea na adhabu zinazotolewa kwa kukiukwa kwake.

Kupitia mafunzo haya, TFRA inalenga kuhakikisha kuwa wadau wote wa sekta ya mbolea wanafanya biashara kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, huku wakitoa huduma bora kwa wakulima na kusaidia katika kufanikisha malengo ya taifa ya kuinua sekta ya kilimo.



Post a Comment

Previous Post Next Post