Wanawake TFRA washiriki Maadhimisho, Siku ya Wanawake Duniani 2025

Mwandishi Wetu,

Wanawake wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wameungana na wanawake wengine nchini kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani leo tarehe 8 Machi, 2025, jijini Arusha chini ya kaulimbiu isemayo “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.”

Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, hatua ambayo imeiwezesha nchi kufikia asilimia 100 ya kujitosheleza kwa chakula na kupunguza tatizo la njaa kwa kiasi kikubwa.

Maadhimisho hayo yaliyoanza tarehe 1 Machi, 2025, yalihusisha makongamano ya wanawake katika Kanda mbalimbali nchini, mijadala ya kuwezesha wanawake kiuchumi, na maonesho ya bidhaa na huduma yaliyofanyika katika viwanja vya kumbukumbu vya Sheikh Amri Abeid.

Wanawake wa TFRA wameshiriki kikamilifu katika maonesho hayo kwa kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na kusajili wakulima katika mfumo wa mbolea za ruzuku ili kunufaika na ruzuku ya mbolea na mbegu inayotolewa na Serikali. 

Kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza umuhimu wa kuziba pengo la kijinsia, kuimarisha usawa wa fursa na kuwezesha wanawake na wasichana katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kilimo ambacho kinaajiri wanawake wengi nchini.



Post a Comment

Previous Post Next Post