TASNIA YA MBOLEA YAWEKA REKODI MIAKA MINNE YA UONGOZI WA RAIS Dkt.SAMIA

 Mwandishi Wetu,

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema, katika kipindi cha miaka minne cha Uongozi wa Awamu ya Sita, Serikali kwa mara ya kwanza imeandaa Mkakati wa Taifa wa Mbolea na Afya ya Udongo (2024 - 2030) ambao tayari umeanza kutumika.

Joel Laurent ametoa kauli hiyo wakati akijibu hoja mbalimbali za Waandishi wa Habari wakati wa wasilisho lake kuhusu mafanikio ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha Miaka minne ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Machi 19, 2025 Jijini Dodoma na kueleza kuwa mkakati huo umeweka malengo na mbinu za kuhakikisha upatikanaji, ufikiaji na matumizi ya mbolea kwa wakulima pamoja na  ustahimilivu wa tasnia ya mbolea nchini.

Aidha,  Joel ameeeleza kuwa Mamlaka hiyo imeanzisha Maabara ya kisasa ya kupima sampuli za mbolea, udongo na tishu za mimea ili kuhakikisha udhibiti wa ubora wa mbolea nchini.

Katika kuhakikisha Matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kurahisisha upatikanaji wa huduma na takwimu muhimu kwenye Sekta ya Kilimo, Joel ameeleza kuwa TFRA imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ambayo yamepunguza muda na gharama za kupata huduma kwa wateja Vilevile, matumizi ya mifumo yamewezesha upatikanaji wa takwimu za uhakika zinazoiwezesha Serikali kuweka mipango ya kuendeleza tasnia ya mbolea na Sekta ya Kilimo kwa ujumla. 

"kupitia Mfumo wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Subsidy System), wakulima wanaendelea kupata  fursa ya kuingizwa kwenye mifumo rasmi ya kifedha kupitia Kadi Janja na fursa ya kupata Hati Miliki za mashamba, uwezeshaji wa huduma za kibenki pamoja  na huduma nyigine muhimu." ameeleza Joel.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa katika kutambua umuhimu wa Sekta ya Kilimo nchini na kuhakikisha pembejeo za mbolea zinapatikana na kumfikia mkulima kwa wakati na kwa gharama himilivu, Mhe. Rais  ameelekeza bandari ya Tanga iweze kutumika  kuhudumia meli zinazoingiza mbolea nchini na zinazosafirishwa kwenda nchi jirani.



Post a Comment

Previous Post Next Post