
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi akifunga Mkutano wa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kaboni Machi 7, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu akitoa neno wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kaboni Machi 7, 2025 jijini Dar es Salaam.
Washiriki wakiwa katika Mkutano wa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kaboni Machi 7, 2025 jijini Dar es Salaam.
…..
Viongozi wa taasisi na mashirika ya umma wamekubaliana kuwa na jukumu la kuweka mazingira bora ya kiutendaji ili biashara ya kaboni na sekta ya mazingira kwa ujumla iweze kukua na kuleta tija nchini.
Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kaboni uliofunguliwa Machi 6, 2025 jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Akifunga mkutano huo Machi 7, 2025, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema, umeleta fursa ya kujadili kuhusu faida za biashara ya kaboni na kuitumia kama vyanzo vya mapato hivyo kuchochea maendeleo endelevu.
Bw. Mitawi amesema kuwa mkutano huo umetoa mwanga wa namna biashara ya kaboni inavyoweza kuwa chombo madhubuti cha kupunguza gesijoto na kuhifadhi mazingira.
“Katika siku hizi mbili za mkutano tumegusia mambo muhimu kama vile fursa zilizopo katika biashara ya kaboni na tumeelewa namna inavyoweza kuleta fedha kwa miradi ya kijamii ikiwemo upandaji wa miti, nishati safi na usimamizi wa ardhi lakini pia nafasi ya taasisi na mashirika ya umma tumekubalina kuwa taasisi zetu zina jukumu la kuweka mazingira bora ya kiutendaji ili sekta hii ikue,” amesisitiza.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mitawi amesema mkutano huo umeibua changamoto katika masuala ya biashara ya kaboni zikiwemo ukosefu wa maarifa na kutoa mapendekezo ya kukabiliana nazo pamoja na kuona namna taasisi hizo zinavyoweza kushirikiana na wadau wa ndani na nje ili kupata masada wa kifedha na kiteknolojia.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imejipanga kuyatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Awali akizungumza wakati wa ufungaji wa mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu amesema mkutano huo ni mwanzo wa ushirikiano kati ya taasisi na mashirika katika kusukuma mbele ajenda ya hifadhi ya mazingira.
Amesema pia, dhumuni la mkutano huo ni kuwa viongozi wa taasisi na mashirika kuwasilisha na kujadiliana kwa pamoja kuhusu fursa wanazokutana nazo katika maeneo yao na kuzifanyia kazi.
Kutokana na hatua hiyo, Prof. Zahabu amesema NCMC iko tayari kutoa ushirikiano kwa kushauri ili kuhakikisha biashara ya kaboni inasonga mbele kwa maendeleo ya taifa.