SERIKALI IMERIDHISHWA NA HALI YA UDHIBITI WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU ITILIMA

 

*******

Na Sixmund Begashe -Itilima

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kutatua changamoto ya mgongano baina ya Wanyamapori na binadamu katika Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu baada ya zoezi maalumu la kuwaondoa Fisi waliokuwa kero kubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

Akizungumza na uongozi wa Wilaya ya Itilima, Maafisa wa Jeshi la Hifadhi na Askari kutoka TAWA, TANAPA na TFS, wanaoendesha operesheni dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan fisi Wilayani Simiyu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amesema, matukio ya fisi kushambulia wananchi kwa sasa yamedhibitiwa.

CP Wakulyamba amebainisha kuwa, matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wanaishi kwa amani na siyo kusumbuliwa na Wanyamapori wakali na waharibifu.

CP. Wakulyamba ameongeza kuwa kazi ya kupambana na changamoto ya Wanyamapori kwenye makazi ya wananchi ni endelevu hivyo wananchi waendelee kutoa ushirikiano haraka kwa Askari wanapoona Wanyamapori wakali kwenye maeneo yao.

“Nichukuwe nafasi hii kuipongeza Serikali ya Wilaya na wananchi wa Itilima kwa kuungana kikamilifu na askari wetu wa Jeshi la Uhifadhi katika zoezi hili muhimu la kulinda usalama wa Maisha ya watu dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu na sasa hali ni shwari.” Alisema CP. Wakulyamba

Aidha CP. Wakulyamba ameuomba uongozi wa Serikali Wilayani Itilima kuendelea kushirikiana na Wizara kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kulinda maeneo yanayohifadhiwa kisheria kwa kutovamia maeneo hayo, maana uvamizi huo ni moja ya sababu inayochochea changamoto ya migongano baina ya binadamu na Wanyama hao.

Aidha, ametoa wito kwa wannchi kutunza mazingira, kuacha kuharibu vyanzo vya mito inayotiririsha maji kwenye maeneo yaliyhofadhiwa ili maji hayo yawafikie Wanyamapori ndani ya hifadhi kuepusha wimbi la wanamyama hao kufuata maji nje ya mipaka ya maeneo yao

Awali Katibu Tawala Wilaya ya Itilima Bi. Mwanana Masumi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa ya kurejesha hali ya amani na utulivu kwa wananchi tofauti na ilivyokuwa siku chache zilizopita ambapo Fisi wasumbufu walisababisha taharuki kubwa kwa wananchi wa eneo hilo

Ziara ya Naibu Katibu Mkuu CP. Wakulyamba katika Mapori ya Akiba yaliyopo chini ya TAWA Wilaya ya Serengeti, Bunda, Bariadi, Itilima na Meatu ililenga kukagua shughuli za uhifadhi, kukutana na kamati ya Usalama ya Wilaya ya Itilima ili kupata taarifa ya hali ya changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu kwa sasa, kuzungumza na Maafisa Waandamizi na Askari wa Jeshi la Uhifadhi kutoka TAWA, TANAPA na TFS wanaofanya kazi ya operesheni ya kunusuru wananchi dhidi ya mnyama hatari Fisi ambaye kwa siku za karibuni amegharimu maisha ya watu.

Katika operesheni hiyo, Askari wamefanikiwa kuwavuna fisi hatarishi na kuwafukuza wengine kwenye makazi ya watu kwa kuwarudisha hifadhini.

Post a Comment

Previous Post Next Post