
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja na viongozi na watendaji mbalimbali wakiangalia magugu maji yaliyozingira Ziwa Victoria. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe na Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa maelekezo wakati wa ziara ya kukagua athari za uwepo wa magugu maji yaliyozingira Ziwa Victoria. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) akitumia boti maalumu kukagua changamoto ya magugu maji yaliyozingira Ziwa Victoria. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe.
……..
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja ameelekeza kufanyika kwa kampeni ya usafi wa mazingira katika miji hususan katika mialo ya Ziwa Victoria ili kukabiliana na athati za kimazingira.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wakurugenzi wote katika halmashauri zinazozunguka ziwa hilo kusimamia zoezi la usafi wa mazingira ili kukabiliana na magugu maji ambayo yanaathiri ziwa.
Ametoa wito huo leo tarehe 10 Machi, 2025 wakati wa ziara ya kukagua eneo la Kigongo katika Ziwa Victoria mkoani wilayani Misungwi Mwanza, lililoathiriwa na viumbe vamizi aina ya magugu maji.
Ziara hiyo iliyowashirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe imelenga kujionea changamoto za kukithiri kwa magugu maji ziwani na kuona namna ya kukabiliana nazo.
Mhandisi Luhemeja amesema uharibifu wa mazingira ni changamoto kubwa inayoleta athari kwa wananchi hivyo inapaswa kupigwa vita kwa kushiriki katika usafi wa mazingira katika miji.
Amewataka wananchi kuacha kugeuza Ziwa Victoria, maziwa mengine, mialo yake, bahari na fukwe zake kuwa ni sehemu ya kutupia taka hali inayochangia uharibifu wa mazingira na kuleta athari.
“Ndugu zangu, suala la mazingra ni vita lazima sote tushiriki kupigana kwani inaathiri moja moja kwa moja wananchi hivyo kila mmoja wetu anapaswa kufanya usafi na kuacha kufanya vitendo vya uchafuzi wa mazingira,” amesisitiza Katibu Mkuu.
Amesema wataalamu kutoka nchini wapata nafasi ya kwenda nchini Uganda kujifunza namna ya kukabiliana na magugu maji ziwani kufuatia taarifa ya Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Jerome Kayombo ambaye amebanisha kuwa nchi hiyo jirani imefanikiwa katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Aidha, Mhandisi Luhemeja amefafanua kuwa uchafu ni mojawapo ya fursa zikiwemo kuzalisha nishati, taka za plastiki zinaweza kurejelezwa na kutengeza bidhaa mbalimbali.
Pia, amesema pamoja na misitu, taka ni sehemu ya mikakati ya kufanya biashara ya kaboni ambayo Serikali inaendelea na jitihada za kuhamasisha jamii ishiriki kikamilifu.
Halikadhalika, Katibu Mkuu Luhemeja amesema Serikali inafanya jitihada za haraka za kukabiliana na changamto ya magugu maji kwani yaathiri sekta ya usafiri wa vivuko kati ya Busisi na upande wa pili na kuathiri vimbe wa ziwani.
Ziara hiyo imeshirikisha pia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Maji na Makatibu Tawala wa mikoa ya Mwanza na Kagera