Na WAF – DODOMA
Katika jitihada za kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini Tanzania ifikapo 2030, Serikali imegawa mashine mpya 185 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7 kwa ajili ya uchunguzi na ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa huo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, leo Januari 6, 2025 kwenye hafla ya ugawaji wa mashine hizo iliyofanyika katika Kituo cha Afya Chamwino, Dodoma iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu katika Halmashauri 76 za mikoa tisa (9).
Waziri Jenista amesema Kifua Kikuu bado ni ugonjwa tishio nchini na ulimwenguni kwa ujumla huku akisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa huo ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote wa Kifua Kikuu Duniani.
“Tanzania ilikadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu 122,000, ikiwa ni sawa na wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000. Aidha, kwa mwaka 2023, Tanzania iliweza kugundua na kuwaweka katika matibabu wagonjwa 93,250 ikiwa ni sawa na asilimia 76 ya wagonjwa 122,000 waliokadiriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwepo nchini” amesema Waziri Mhagama.
Amesema kuwa hali hiyo imeleta msukumo mkubwa ndani ya Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta katika kuongeza juhudi za kupambana na Kifua Kikuu.
“Leo tunazindua mashine za kisasa 75 aina ya GeneXpert zinazotumika katika ngazi ya Hospitali, na mashine 110 aina ya Truenat ambazo zimetengenezwa kuwezesha kufanya kazi hadi katika ngazi ya Zahanati. Mashine hizi zimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 7 na zitasambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na mikoa miwili (2) upande wa Zanzibar,” amefafanua Waziri Mhagama
kwa kuzindua mashine hizo, Tanzania inaendelea kuimarisha mtandao wa huduma za uchunguzi na ugunduzi wa vimelea vya Kifua Kikuu kwa njia ya vinasaba ambapo sasa kutakuwa na jumla ya mashine 569 zenye uwezo wa kupima vimelea vya Kifua Kikuu pamoja na usugu wa dawa kutoka mashine 384 zilizokuwepo mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 48.
Katika hatua nyingine Waziri Jenista amezindua Mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu kwenye Halmashauri 76 kutoka Mikoa 9 amabyo kwa 2024 imeonyesha kuwa na kiwango kidogo cha uibuaji wa wagonjwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Waziri Jenista ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kagera, Mara, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu na Tanga.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe.Janeth Mayanja ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.
Amesema kuwa mashine hizo zilizotolewa zitakwenda kusaidia katika utambuzi wa mapema wa wagonjwa wa Kifua Kikuu hivyo kuibua watu wengi zaidi wanaogua ugonjwa huo na kupata tiba mapema.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Ahmad Makuwani amesema kuwa licha ya ugonjwa huo kuendelea kuwa tishio, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na Kifua Kikuu ikiwa ni miongoni mwa nchi sita (6) zinazofanya vyema katika mapambano.
Dkt. Makuwani amesema kuwa juhudi kubwa sasa zinaelekezwa katika uibuaji wa wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya matibabu hasa kwenye vifaatiba, hivyo sasa tuna jukumu la kutoacha mtu nyuma kwenye mapambano hayo na kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030.