Serikali ya Tanzania imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana kwa pamoja katika kulinda mifumo ikolojia ya dunia dhidi ya ukame ambao umeleta tishio kwa mazingira.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akishiriki Mkutano wa 16 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame jijini Riyadh, Saudi Arabia uliofunguliwa leo Desemba 02, 2024.
Amesema pamoja na changamoto ya ukame, Serikali imejenga mifumo thabiti ya kuhimili hali ya ukame kwa ambao umeleta tishio kwa maisha, usalama wa chakula na upatikanaji wa maji nchini.
Mhe. Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilizindua Mpango Kabambe wa Mazingira (2022-2032) iikiwa ni jitihada za kukabiliana na changamoto ya ukame.
Naibu Waziri Khamis Khamis amefafanua kuwa Mpango Kabambe wa Mazingira umejumuisha sekta mbalimbali zikiwemo maji, kilimo na misitu ambazo ni muhimu kwa binadamu.
Amesema kupitia sekta hizo Serikali imewekeza katika kilimo kinachozingatia hali ya hewa ili kuhakikisha inakuwepo mifumo inayostahimili ukame na mifumo ya tahadhari ya mapema ili kutoa taarifa kwa wakati kwa jamii zilizo hatarini.
Ametaja juhudi zingine kuwa ni mipango ya uhifadhi wa mabonde na uendelezaji wa miundombinu ya maji ili kuboresha usalama wa maji
na matumizi bora na kukuza ufumbuzi wa nishati safi ili kupunguza ukataji miti na kuboresha ufanisi wa nishati.
“Tunapoendelea na juhudi hizi, tunaomba jumuiya ya kimataifa itusaidie katika kuimarisha upatikanaji wa fedha kupitia Mfuko wa GCF, kuongeza miradi kama vile Mradi wa Kustahimili Hali ya Hewa wa Simiyu, ambao huchangia upatikanaji wa maji katika mikoa yenye ukame,” amesema.
Mhe. Khamis ameomba pia uwezeshaji katika kukuza teknolojia na kujenga uwezo wa udhibiti wa ukame kitaalamu pamoja na taratibu za kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza kwa ajili mipango mikubwa ya kustahimili ukame.
Mkutano wa 16 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame unatarajiwa kuhitimishwa Desemba 13, 2024