Mwandishi Wetu,
Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la wawakilishi Zanzibar imeitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ya Zanzibar kuharakisha mchakato wa kuingia makubaliano na Kampuni ya Mbolea Minjingu inayozalisha mbolea asilia ili kuounguza uagizwaji wa mbolea nje ya Nchi.
Wito huo ulitolewa Novemba 10, 2024, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mtumwa Peya Yussuf wakati wa ziara iliyoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), iliyolenga kuwajengea uelewa na kujifunza namna bora wanayotumia katika kuzalisha mbolea kwa kwa kuzingatia usalama wa mazingira na kuimarisha afya ya udongo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo, Umwagiliaji, Mali asili na Mifugo Zanzibar ,Ali Khamis Juma, aliye ambatana na kamati hiyo amesema tayari Wizara yake imetoa bure Maghala manne kwa kampuni ya Minjingu ili kuhifadhi mbolea na kurahisisha upatikanaji na usambazaji wa mbolea hiyo mjini Zanzibar kabla ya Mwezi Januari Mwaka 2025.
‘‘lengo la Wizara ya Kilimo, Mifugo, Umwagiliaji, Mali asili na Mifugo Zanzibar ni kupunguza uagizaji wa mbolea za kemikali viwandani kwa zaidi ya asilia 50 kuanzia Januari mwaka 2025’’ Juma aliongeza.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent ,Meneja wa TFRA Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe amesema Mamlaka ipo tayari kushirikiana na Wizara hiyo katika kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu masuala yanayohusu Huduma Za Udhibiti wa Mbolea.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni mkakati thabiti wa Wizara ya Kilimo zanzibar kuongeza matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa Zanzibar ili kuongeza tija na uzalishaji utakaoleta usalama wa chakula nchini Zanzibar.