SERIKALI YASAJILI MIRADI 63 YA KABONI

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imesajili miradi 63 ya biashara ya kaboni kupitia sekta mbalimbali.

Mhe. Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Novemba 06, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Amani Mhe. Abdul Yussuf Maalim aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuongeza wigo wa biashara ya kaboni ili kupunguza uharibifu wa ukataji wa misitu nchini. 

Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis ametaja sekta zilizo katika miradi iliyosajiliwa ni pamoja na Kilimo (asilimia 8), Nishati (asilimia 33), Misitu (asilimia51), Mifugo (asilimia 5) na Usimamizi wa taka (asilimia 3).

Amesema kati ya miradi iliyosajiliwa kupitia Sekta ya Misitu ni minne inahusisha shughuli za upandaji miti, miradi 20 ni kwa ajili ya kupunguza uharibifu na upotevu wa misitu na miradi mitano ni kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili. 

Aidha, Mhe. Khamis ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 2034) ambao unahamasisha matumizi ya nishati safi za kupikia ikiwemo gesi asilia, nishati jadidifu, mkaa mbadala na umeme ambazo zinaweza kuchangia katika Biashara ya Kaboni na kupunguza matumizi ya kuni na ukataji wa misitu. 

Halikadhalika, amesema Serikali imeandaa na inatekeleza Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu 2024 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu (2024 2034).

Mheshimiwa Mwenyekiti katika Sera hii ya Taifa ya Uchumi wa Buluu tumeweka mikakati ya kuhamasisha matumizi ya hati fungani za buluu na biashara ya kaboni katika shughuli za rasilimali za Uchumi wa Buluu kwa lengo la kuongeza wigo wa biashara ya kaboni nchini ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira, amesema. 

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali inachukua mipango madhubuti kuhakikisha misitu inakuwa sehemu ya mapato kupitia biashara ya kaboni katika vijiji, shehia na wilaya kwa kuwashirikisha wananchi katika kuihifadhi.

Akijibu maswali la nyongeza la Mhe. Maalim kuhusu hatua Serikali inachukua katika kuitunza misitu na Zanzibar imenufaikaje na biashara ya kaboni, Mhe. Khamis ameeleza kuwa 

Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kutoa elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo wabunge kuhusu fursa zinazopatikana katika biashara ya kaboni kwa upande wa Zanzibar pamoja na kuwaunga mkono katika kuandaa kanuni za biashara ya kaboni.

Post a Comment

Previous Post Next Post