PROF. MKENDA AHIMIZA USIMAMIZI THABITI ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI NCHINI

 


Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Prof Adolf Mkenda (Mb), amesema uthabiti katika usimamizi wa utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yenye ubora, ni kichocheo cha kuvutia uwekezaji nchini.

Mhe. Prof. Mkenda amebainisha hayo jana tarehe 28 Oktoba, 2024 kwenye hafla ya uzinduzi iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kufuatia uteuzi alioufanya Mhe. Waziri wa Waheshimiwa Wajumbe wapya wa Baraza la Uongozi la NACTVET.

Akizungumzia mageuzi yaliyofanywa na Serikali chini ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uga wa elimu nchini, Prof. Mkenda amesema suala la uimarishaji ubora halina mbadala katika kuhakikisha upatikanaji wa nguvukazi yenye ujuzi na umahiri.

Prof. Mkenda ameweka mkazo kwa wajumbe wa Baraza la Uongozi kutosita kuishauri Serikali kuhusu maboresho katika utoaji mafunzo ya amali kwa msisitizo kwenye eneo la ubora wa mitaala kwa lengo la kuhakikisha viwango vya mafunzo yanayotolewa na ubora wa wahitimu vinaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira kitaifa na kimataifa.

“Tuna wajibu wa kuhakikisha tunakidhi matarajio ya Watanzania wanaojiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa na kuendesha maisha yao,” amesisitiza.

Waziri Mkenda ameipongeza NACTVET kwa kushiriki kikamilifu katika jukumu la kuwezesha utoaji wa elimu ya sekondari mkondo wa amali, ambapo amesema wahitimu wa mkondo wa amali watapata cheti kutoka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) na cheti kutoka NACTVET kinachotambulisha mafunzo ya amali.

Amebainisha kwamba Serikali iko mbioni kukamilisha ujenzi wa vyuo vya kati vya ufundi (polytechnics) vinne katika mikoa ya Kigoma, Mwanza, Mtwara na Zanzibar ili kutoa nafasi kwa wale wanaohitimu kidato cha nne kujiunga na vyuo hivyo ili kupata mafunzo ya umahiri katika ufundi.

Wakati huo huo, Mhe. Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTVET, Bi. Bernadeta Ndunguru, amesema Baraza hilo limejipanga kikamilifu kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uwajibikaji mkubwa hasa kwa kuzingatia kuwa wajumbe wa Baraza hilo wanatoka katika sekta muhimu ambazo ni wadau wakubwa wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Bi. Ndunguru amepongeza hatua ya NACTVET kuwajengewa uwezo waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Uongozi mapema mwezi Oktoba, juu ya shughuli zinazofanywa na NACTVET ikiwemo kuzifahamu Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya Baraza ili kuwaongezea ujuzi utakaoleta ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kuisimamia NACTVET yaliyo mbele yao.

Awali, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Adolf Rutayuga alimhakikishia Waziri, Prof. Mkenda kuwa Menejimenti ya NACTVET itatoa ushirikiano wa karibu kwa Baraza la Uongozi katika utekeleza majukumu yake ili kuhakikisha malengo ya Baraza yanatimizwa kwa ufanisi, uwazi na uadilifu.

Baraza la Uongozi NACTVET chini ya uongozi wa Mhe. Mwenyekiti Bi. Bernadetta Ndunguru litahudumu kwa muda wa miaka mitatu (2024 – 2027) ambapo wajumbe wake ni Qs. Samwel Nyantari Marwa kutoka Bodi ya Wakandarasi Tanzania (CRB), Dkt. Mwajuma Ibrahim Lingwanda kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia (WyEST), Dkt. Abdallah Shaban Ngodu kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Telemu J. Kassile kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na CPA (T) Angyelile V. Tende kutoka Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA).

Wengine ni Bi. Mariam G. Mwanilwa kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-UUB), Mha. Prof. Sylvester M. Mpanduji kutoka Taasisi ya Uendelezaji Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO), Bi. Suzanne Ndomba-Doran kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Prof. Kennedy Aliila Greyson Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Mmoja wa wajumbe wa Baraza la Uongozi NACTVET, Qs. Samwel Nyantari akitoa neno la shukrani mara baada ya uzinduzi wa Baraza
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTVET, Bernadetta Ndunguru akizungumza muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa Baraza hilo jijini  Dar es Salaam.


Baadhi ya picha za  wajumbe na watendaji wa NACTVET wakati wa uzinduzi  wa  Baraza la Uongozi NACTVET ,jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akiwa katika picha za pamoja za makundi mbalimbali mara baada ya kuzindua Baraza la Uongozi la NACTVET  jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

Previous Post Next Post