Tanapa yazindua Kampeni Twenzetu Kileleni kwa msimu wa nne

 Na Mwandishi Wetu

KAMPENI ya msimu wa nne wa Twenzetu Kileleni imezinduliwa rasmi na inakwenda sanjari na Kauli Mbiu  inayosema 'Stawisha Uoto wa Asili Tanzania, Okoa Barafu Mlima Kilimanjaro'.

Lengo la kampeni hiyo itakayoenda hadi Desemba 4,mwaka huu  ni kusheherekea  miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika ambao Kila mwaka usheherekewa Desemba Tisa.

Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam Leo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo na Biashara wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Jully, Lymo, amesema watanzania zaidi ya 500 watasherekea siku hiyo katika kilele cha Mlima Kilimanjaro'.

  “Katika sura ya Utalii, TANAPA imekuwa ikitumia fursa hii ya maadhimisho ya siku ya uhuru kuhamasisha watanzania kupanda mlima Kilimanjaro na kutangaza vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hii kupitia kampeni ya “Twenzetu kileleni” .Lengo la kampeni hii ni kuhamasisha Watanzania kupanda mlima ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika”.

 “Nichukue nafasi hii kuwahamasisha Watanzania wenzangu kushiriki upandaji huu ikiwa ni kuonyesha uzalendo na kupenda vivutio vyetu.

"Amesema kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu kampuni tatu zimejitokeza kushiriki katika kampeni hiyo, ambazo ni ZARA Tours, African Zoom na African Scenic. 

Ameongeza kuwa kampuni ya ZARA TOURS watatumia njia ya Marangu kama ilivyozoeleka, African Zoom watatumia njia ya Machame na African Scenic watatumia njia ya Lemosho ambapo idadi ya siku za kupanda mlima huo ni sita kwa njia ya Marangu.

 Pia siku saba kwa njia ya Machame na kwa Lemosho itakuwa siku nane na gharama za kupanda mlima zitakuwa ni shilingi 1,55,000 kwa njia ya Marangu, shilingi 1,830,000 kwa njia ya Machame na 2,000,000 kwa njia ya Lemosho. 

 Naye, Mhifadhi Mkuu Mapinduzi Mdesa kutoka Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro aliwataka watanzania wote kujitokeza katika kuadhimisha sherehe hizo za uhuru katika kilele kirefu zaidi barani Afrika pamoja na kushiriki katika juhudi za kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro.

 "Kama mwenyeji wa mlima niwakaribishe watanzania kuja kushiriki nasi katika sherehe hizi za Uhuru katika Paa la Afrika lakini tunajukumu la kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro kwa kustawisha uoto wa asili kwenye maeneo yetu”

 Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kuwa chanzo cha barafu kuyeyuka Mlima Kilimanjaro ni uwepo wa pepo kavu zinazotokea baharini na maeneo mengine ya nchi zikifika kwenye ile barafu ya Mlima Kilimanjaro zinapelekea Barafu ile kupungua ukubwa wake na kutoa rai ya kukijanisha Tanzania kwa kupanda miti ya asili ili pepo zinazotoka kwenye fukwe ziende na unyevu na kusaidia barafu iendelee kuwepo.

 Historia inaonyesha kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na utaratibu wa kuadhimisha sherehe za Uhuru wa Tanganyika tangu ulivyopatikana mwaka 1961.

Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kwa kupandisha bendera ya nchi yetu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Kupanda Mlima Kilimanjaro kwa sasa sio tu ndoto ya wageni kutoka mataifa ya mbali, bali ni nafasi kwa Watanzania kuupanda mlima wao wenyewe, kujivunia urithi wao, na kusaidia juhudi za kuhifadhi uoto wa asili na mazingira ya Tanzania kwa ujumla.



Post a Comment

Previous Post Next Post