WAHIFADHI TFS-SHAMBA LA MITI SAOHILL WAPONGEZWA KWA UTENDAJI KAZI MZURI

 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewapongeza wahifadhi Shamba la Miti la Miti Saohill kwa utekelezaji mzuri wa majukumu alipotembelea kuona shughuli zinazofanyika katika shamba hilo leo Septemba 10, 2024.

Katika ziara hiyo, Mhe. Chana amepokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya uendelezaji wa shughuli za shamba kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa Shamba PCO. Tebby Yoramu ikiwa ni uzalishaji wa miche, uvunaji wa miti na utomvu, ufugaji nyuki na utalii ikolojia.

Kwa upande mwingine Waziri Chana amehimiza wahifadhi kuwa na ushirikiano baina yao na wananchi ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwa na maadili mema katika utendaji wao lakini pia kuwepo mfumo wa upatikanaji wa taarifa za maeneo yote ya shamba kwa ukaribu zaidi.

Aidha, amewataka wahifadhi kuendeleza juhudi za kulinda misitu dhidi ya matukio ya moto ambayo yanayotokea hususani katika kipindi hiki cha kiangazi.

 "Licha ya kuwepo kwa changamoto ya moto katika maeneo ya hifadhi tunapaswa kutumia teknolojia za kisasa katika kupambana na matukio ya moto ikiwepo matumizi ya ndege zisizo na rubani (Drones) ili kurahisisha utambuzi wa matukio ya moto kwa haraka" amesema Waziri Chana.

Pia amesisitiza kuwepo kwa usimamizi mzuri wa rasilimali za misitu na nyuki katika maeneo ya hifadhi ili kuepusha migogoro inayotokana na uvamizi wa maeneo unaofanywa na wananchi katika hifadhi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Bw. Deusdedit Bwoyo amesema kuwa Wizara kupitia Idara ya Misitu na Nyuki itaendelea kuhakikisha kuwa inatoa ushirikiano ili kuhakikisha kunakuwa na utendaji mzuri zaidi na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokwamisha utakelezaji wa baadhi ya majukumu ya ki uhifadhi.





Post a Comment

Previous Post Next Post