TPDC KUUZA GESI NCHI JIRANI

 

Na Sophia Kingimali.

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inampango wa kuuza gesi katika nchi jirani ambapo hatua hiyo itaifanya nchi kuwa tegemeo la nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mussa Makame, kaimu Mkurugenzi wa fedha na Utawala Ahmad Massa amesema tayari seeikali imeshaingia makubaliano na nchi hizo ambazo ni Uganda,Kenya,Congo na Zambia.

Amesema gesi hiyo itaweza kufika kwa wateja hao kwa njia ya bomba ama LNG/Mini LNG ambapo tayari TPDC imeshasaini mikataba ya ujenzi wa mitambo hiyo.

Aidha Massa amesema kuwa TPDC sasa wanaenda kushiriki moja kwa moja kwenye sekta ya kilimo ambapo kwa kutumia gesi asilia kitaenda kuzalisha mbolea ya UREA.

“Tunaamini kuwa kiwanda kitakachoenda kujengwa kwa kushirikiana na wenzetu wa kampuni ya ESSA kutoka Indonesia katika mkataba tuliosaini Julai 31,2024 kitaenda kuwa mkombozi katika sekta ya kilimo lakini pia kitalifanya Taifa kuwa tegemeo la mbolea katika ukanda wa Kusini mwa Afrika”,Amesema.

Akizungumza katika Semina ya wanahabari iliyoandaliwa na shirikia hilo ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu maswala ya mafuta na gesi amewataka wanahabari nchini kujifunza zaidi kuhusu mradi wa bomba la kusafirishia mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga.

Amesema mradi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya EACOP umeundwa na wanahisa wanne yaani TPDC,UNOC,CNOOC na Total Energies ambapo utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 30.

“Asilimia 30 zilizofikiwa ukihisisha ujenzi wa kiwanda cha kuweka mifumo ya upashaji moto wa vipande vya mabomba,ujenzi wa makambi ya wafanyakazi na uhifadhi wa vifaa,ujenzi wa kituo cha kuhifadhi mafuta pamoja na jeti katika eneo la bandari jijini Tanga”,Amesema.

Pia,amesema kuwa TPDC kwa kushirikiana na AR Petrolium wanatarajia kuanza uzalishaji wa gesi asilia katika eneo la Ntorya ambapo wataanza kuzalisha futi za ujazo milioni 60 kwa siku na kupeleka kwenye kiwanda cha kuchakuta gesi asilia cha Madimba Mkoani Mtwara.

Katika kuzingatia matumizi ya nishati safi ya kupikia Mhandisi Mwandamizi idara ya biashara ya mafuta na gesi Anthony Karombo amesema jumla ya nyumba 1511 zimeunganishwa na zinatumia gesi asilia nchini kupitia miundombinu katika mikoa ya Dar es salaam 877,Mtwara 425 na Lindi nyumba 209.

Aidha Mhandisi Korombo ameongeza kuwa gesi asilia pia inatumika uendelezaji na uzalishaji wa bidhaa kwenye viwanda zaidi ya 50 ambavyo vimeunganishwa na gesi asilia katika mkoa wa Dar es salaam,Pwani na Mtwara. 

Post a Comment

Previous Post Next Post