Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameeleza kuwa Wizara yake itahakikisha maelekezo ya Serikali yaliyotolewa hivi karibuni kwa wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kuhusiana na uboreshaji wa huduma za jamii yanatekelezwa.
Mhe. Chana ametoa kauli hiyo alipotembelea makao makuu ya ofisi za Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kuongea na Menejimenti ya NCAA na kusisitiza kuwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na uratibu) William Lukuvi aliyoyatoa kwa wananchi wa Ngorongoro Agosti, 2024 ikiwemo utoaji wa vibali vya kuboresha huduma za jamii, kuongeza muda wa wananchi kuingia hifadhini kutoka saa 10:30 jioni hadi saa 12, usalama wa wananchi ndani ya hifadhi, na kuongeza uhusiano baina ya NCAA na wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi.
Katika kuimarisha shughuli za ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na Misitu,Waziri Chana amezielekeza taasisi za uhifadhi kuongeza ubunifu na juhudi katika matumizi ya teknolojia za kisasa zinazoendana na wakati uliopo kwa ajili ya kuimarisha usalama wa rasilimali hizo kwa maslahi ya taifa na vizazi vijavyo.
Pia amezitaka taasisi na mashirika yote chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii yenye Bodi kuzitumia kikamilifu Bodi hizo ili kuongeza ufanisi wa kazi.
Katika hatua nyingine Mhe. Waziri Chana ameeleza kuwa zoezi la kuelimisha wananchi na kuwahamisha kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda maeneo yaliyotengwa na Serikali iko palepale.
Ameielekeza menejimenti ya NCAA kuendelea kutekeleza jukumu la kuwaelimisha wananchi ili wahamie kwa hiari kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uhifadhi na kuboresha ustawi wa maisha yao nje ya hifadhi.
Akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kati ya tarehe 18- 23 agosti, 2024, Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii (Maliasili) CP. Benedict Wakulyamba ameeleza kuwa wananchi waliandamana na kutoa madai yao katika hali ya amani na utulivu bila kuleta athari katika eneo la hifadhi ambapo pamoja na changamoto zilizojitokeza shughuli za utalii ziliendelea.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi, NCAA, Dkt. Elirehema Doriye amemueleza Mhe. Waziri kuwa utekelezaji wa shughuli za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii zinaendelea vizuri na uongozi wa NCAA unaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na huduma zingine kwa wageni wanaondelea kutembelea hifadhi kila siku.