
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dk. Ladislaus Chang’a akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024.
xxxxxxxx
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dk. Ladislaus Chang’a amesema kuwa maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
“Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, Mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari katika maeneo mengi na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2024, Aidha, aliongeza kuwa ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Machi 2024.” amesema Dk. Chang’a.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dk. Chang’a amesema kuwa vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza kusababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.
Katika hatua nyingine, Dk. Chang’a ameshukuru Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na hivyo kuiwezesha TMA kufikia hatua ya kuongeza usahihi wa utabiri.
Dk. Chang’a amesisitiza jamii kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA kwa vile ni za uhakika, na usahihi wa msimu wa Vuli 2023 ulikuwa asilimia 98.