TRA YAZINDUA KAMPENI YA TUWAJIBIKE

 NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua rasmi Kampeni ya Tuwajibike  inayolenga kuwahamasisha walipakodi na wananchi kwa ujumla  kuhusu wajibu wao wa kutoa na kudai risiti sahihi za EFD.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo amesema kampeni hiyo inayoanza  mwezi huu Mei, 2023 ni endelevu.

"Kampeni hii ya Tuwajibike ni endelevu na inaanza rasmi mwezi huu wa tano ikiwa na malengo yafuatayo; kuwakumbusha na kuwasisitiza wauzaji wa bidhaa na watoa huduma nchi nzima kuwajibika kwa kutoa risiti halali ya EFD kila wanapouza bidhaa au kutoa huduma mbalimbali,  kuwakumbusha na kuwahamasisha wanunuzi wa bidhaa na huduma kote nchini kuwajibika kudai risiti halali ya EFD pamoja na kuzikagua ili kujiridhisha kuwa inakidhi vigezo vyote muhimu," amesema Bw. Kayombo.

Malengo mengine ya kampeni hiyo kwa mujibu wa Bw. Kayombo ni kufuatilia utoaji wa risiti halali za EFD nchi nzima pamoja na kuchukua hatua kwa wauzaji wasiofuata sheria katika utoaji wa risiti halali za EFD ikiwemo kutokutoa risiti ya EFD na kutoa risiti yenye  kiwango cha chini kulingana na thamani halisi ya bidhaa au huduma, wafanyabiashara tofauti kutumia risiti moja wakati wa kusafirisha mizigo pamoja na kuuza risiti pasipokuwa na manunuzi yoyote.

Akizungumzia suala la risiti halali ya EFD, Bw. Kayombo amesema kuwa risiti halali inatakiwa kukidhi vigezo vikuu vinne ambavyo ni Jina la biashara, tarehe halisi ya mauzo, kiwango halisi cha pesa kilichotolewa kwa  bidhaa au huduma na  jina au TIN ya mnunuzi au vyote kwa pamoja.

"Ukiachilia mbali vigezo hivyo vya risiti halali, napenda kuwakumbusha kuwa, adhabu ya mfanyabiashara atakaebainika kutokutoa risiti halali ya EFD au kufanya udanganyifu atatozwa faini ya shilling 3,000,000 mpaka shilling 4,500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja," alifafanua Bw. Kayombo na kuongeza kuwa, kwa upande wa mnunuzi atakayebainika kufanya manunuzi bila ya kudai risiti halali ya EFD atatozwa faini ya shillingi 30,000 mpaka 1,500,000.

"Faini hizo zipo kisheria na kazi yetu ni kusimamia sheria hivyo natoa  wito kwa wafanyabishara wote kuwajibika kwa kutoa risiti halali za EFD bila ya kushurutishwa na wanunuzi nao wanatakiwa kudai risiti halali za EFD kwa kila manunuzi watakayoyafanya ili kuepuka usumbufu usio wa lazima," alisema Mkurugenzi Richard Kayombo.  
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo,  amekutana na waandishi wa habari na kutangaza rasmi uzinduzi wa "Kampeni ya Tuwajibike" inayolenga kuwahamasisha walipakodi na wananchi kwa ujumla  kuhusu wajibu wao wa kutoa na kudai risiti sahihi za EFD. Mkutano huo umefanyika leo tarehe 2/5/2023 katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.
.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa "Kampeni ya Tuwajibike" inayolenga kuwahamasisha walipakodi na wananchi kwa ujumla  kuhusu wajibu wao wa kutoa na kudai risiti sahihi za EFD. Mkutano huo umefanyika leo tarehe 2/5/2023 katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

Previous Post Next Post