No title

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaasa wachimbaji wadogo wa dhahabu kutumia teknolojia mbadala wa miti katika shughuli zao.


Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo wakati akishiriki katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na Kituo cha Runinga cha ITV Aprili 10, 2023 jijini Dar es Salaam.

Amesema ni kweli uchumi unaotokana na uchimbaji wa madini ni muhimu lakini wachimbaji katika maeneo mbalimbali nchini wanapaswa kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Dkt. Jafo amesema kumekuwa na uharibifu wa mazingira katika maeneo ambayo shughuli hizo zinafanyika ambapo wachimbaji wadogo wanakata miti kwa ajili ya kujengea mashimo hivyo ni wakati sasa kwa wachimbaji hao kuanza kutumia chuma.

Pamoja na changamoto hiyo ya ukataji miti ametoa pongeza kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha zoezi la upandaji miti kwa wachimbaji na wananchi kwa ujumla.

Pia, Waziri Jafo amezungumzia suala la uchimbaji wa mchanga hususan katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo amesema una changamoto ya wachimbaji kufanya shughuli bila kufuata utaratibu hali inayosababisha uharibifu wa mazingira.

“Ni kweli tuna changamoto kubwa ya uchimbaji wa madini ya mchanga na watu wanaacha makorongo baada ya kuchimba kwa mfano kule Kigamboni wanaharibu mazingira, wapo baadhi ya watu tunashukuru wanafukia mashimo baada ya uchimbaji.

Hata hivyo, Dkt. Jafo amefafanua kuwa shughuli yoyote ya uchimbaji lazima ipate kibali cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

“Baadhi ya watu wanaharibu kingo za mito kwa kuchimba mchanga bila kufuata utaratibu sasa wanatakiwa kuunda vikundi wapewe utaratibu rasmi wa kusafisha mito ili kupeuka kuharibu mazingira,” amefafanua.

Post a Comment

Previous Post Next Post