BODI YA UTALII YATOA MSAADA KWA JAMII

 Na. Mwandishi wetu, DARA ES SALAAM

Bodi ya Utalii Tanzania imetoa msaada wa baiskeli kwa wenye ulemavu ikiwa ni mwendelezo wa kushirikiana na jamii hususani katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo pia imetoa msaada vyakula ikiwa pia ni katika kuchangia maandalizi ya mashindano ya Quran yanayotarajiwa kufanyika hapo kesho.

Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Damasi Mfugale amewasilisha msaada wa Baiskeli, fimbo kwa ajili yakutembelea watu wenye ulemavu, kofia na mafuta kwa ajili ya walemavu wa ngozi pamoja na vyakula ikiwa ni maandalizi kuelekea katika mashindano ya kusoma Quran 

Mfugale ameeleza kuwa Bodi hiyo inayohusiana na mambo ya utalii inayo nafasi muhimu ya kuenzi na kushirikiana na jamii kwa kuwa utalii ambao wamekuwa wakiutangaza hauleti tija kwa serikali pekee lakini pia unagusa maisha ya wananchi.

“Tukio la leo tumefanya kusaidia hasa watu wenye changamoto ya ulemavu mbalimbali, tumetoa baiskeli tatu na wheelchair mbili, vilevile kwa wenzetu waislam tumetoa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele pamoja na mafuta kwaajili ya kuchangia mashindano ya Quran yatakayofanyika hapo kesho.” Amasema Mfugale

Mfugale ameongeza, “hata sisi tuna jukumu la kuhakikisha chochote chenye changamoto katika jamii zetu tunachukua nafasi yetu katika kuhakikisha kwamba tunaisaidia jamii yetu.”

Ameongeza kuwa, watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo na kwamba dhana ya mtalii siyo mtu kutoka nje ya nchi pekee.

“Najua kuna changamoto hasa kwa watu wenye ulemavu wanaweza kushindwa kufikia vivutio vyetu, lakini sisi Bodi ya utalii tuna mikakati huko mbele ya kuhakikisha tunaongeza idadi ya watalii hasa watalii wa ndani tutakuwa tunaangalia pia hiyo changamoto ili waweze kufikia vivutio mbalimbali vya nchi yetu.” Amesema Mfugale

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Taasisi inayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu ya Equal Right Omar Sozigwa ameishukuru Bodi ya Utalii kwa kuwasaidia na kuwaomba wasiishie hapo.

“Kwasababu hivi ni vifaa tunatumia lakini kuna muda vitakuwa vinakwisha, tunaomba kwa hilo mtupokee tena pindi ambapo tunakuja kutoa maombi yetu basi msituchoke kwasababu wenye mahitaji maalum huwa tuna changamoto sana hususani katika suala la vifaa kama hivi, kwahiyo tutakuja tena kipindi ambapo vimeisha msituchoke,” amesisitiza Makamu mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Said Shabaan Naibu Imam kutoka Buguruni Sukita ameishukuru Bodi ya Utalii na kusema kuwa kupitia msaada huo maandalizi ya mashindano ya Quran yatakamilika kwa wakati.

 Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini Damasi Mfugale akikabidhi msaada wa vyakula na baiskeli za magurudumu, wa pili kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi inayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu ya Equal Right Omar Sozigwa
 Makamu Mwenyekiti wa Taasisi inayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu ya Equal Right Omar Sozigwa akimshukuru Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii mara baada ya kupokea vifaa vya msaada vilivyotolewa na Bodi hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post