MCHENGERWA AFUNGUA KITUO CHA KISASA CHA HABARI SERENGETI, AAGIZA KUANZISHWA KWA TUZO ZA UTALII

 


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo amefungua Kituo cha Habari cha kisasa chenye hadhi ya kimataifa kitakachotumika kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo kwenye mbuga na hifadhi zote nchini huku akisisiza kuwa Tanzania lazima ijitangaze na kuwapata watalii zaidi ya lengo la milioni 5 ifikapo 2025 kwa kuwa imebarikiwa kuwa na vivutio vingi ambavyo havipatikani sehemu nyingi duniani isipokuwa Tanzania pekee.

Akifungua kituo hicho leo Machi 10, 2023 kilichojengwa katikati ya Mbuga ya Serengeti kwa ufadhili wa Serikali ya Korea kupitia Shirika la KOICA amefafanua kuwa ili kuvitangaza vivutio hivyo ni lazima kila mdau wa sekta ya utalii nchini kushiriki kikamilifu katika kuvitangaza badala ya kuiachia Serikali peke yake.

“ Wakati ni sasa kila mdau atoke, iwe ni mwekezaji wa mahoteli iwe ni makampuni ya usafirishaji, tusiridhike na idadi ndogo ya watalii tunayoipata, twende kila bara kama tulikuwa tumeishia Marekani twende Ulaya na Uarabuni kuwaletee watalii”. Amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Amehoji kama Rais wa Jamhuri ya Muungano aliamua kutoka ofisini na kwenda kuitengeneza Filamu ya Royal Tour ambayo imeifungua Tanzania duniani, je watumishi wa Serikali ni nani hadi wasitoke kuvitangaza vivutio hivyo.

Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Hassan Abbasi ambaye pia amehudhuria uzinduzi huo na Naibu wake Anderson Mutatembwa kuanda utaratibu kila mwaka utakao watambua watanzania ambao wanaoitangaza na kuwaleta wageni nchini ili kuwatunikia vyeti vya kutambua mchango wao.

Pia ameagiza kuanzisha matamasha ya utoaji tuzo za filamu zinazotangaza vivutio vilivyopo nchini kwa kushirikiana na wadau wengine kama Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo akitolea mfano wa uwepo kwa Tamasha la Wanyama la Serengeti (Serengeti Wildlife Film Festival) ambao utasaidia kutangaza vivutio vya utalii na utachochea uandaaji wa filamu bora za utalii.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Generali Mstaafu George Waitara ameishukuru KOICA kwa msaada huo na kumhakikishia Waziri Mchengerwa kukitumia kikamilifu kituo hicho cha Habari kwa lengo lililokusudiwa.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Korea kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii.

Ametoa wito kwa KOICA kuendelea kushirikiana na Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) katika kuandaa vionyeshwa bora (Quality contents), kutunza na kuboresha majengo na vifaa vya kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuwajengea uzoefu na wataalam kwenda katika mataifa mbalimbali ili kujifunza mataifa hayo yamewezaje kufanikiwa.

Amefafanua kwamba kumekuwa na baadhi ya mataifa duniani ambayo hayana vivutio vya utalii lakini yamefanikiwa kuwa na watalii wengi na kuchangia mapato makubwa kwenye uchumi wa mataifa yao ukilinganisha na Tanzania.

Balozi wa Korea nchini, Mhe. Kim Sun Pyo amemhakikishia Mhe Mchengerwa kuwa Serikali yake itaendelea kuimarisha mahusiano katika sekta ya utalii.      

Post a Comment

Previous Post Next Post