Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Jenerali Venance Mabeyo ( Mstaafu) amesema Uzinduzi wa Makumbusho ya Kisasa ya Kimondo cha Mbozi utachagiza fursa za kiuchumi kwa Wananchi wa Mkoa wa Songwe na Taifa kwa ujumla.
Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 4, 2023 wakati akizindua Makumbusho hiyo iliyopo katika eneo la Kimondo katika kijiji cha Ndolezi kata ya Mlangali wilayani Mbozi
Katika hotuba yake Jenerali Mabeyo amesema kuwa kwa Kijiji hicho kupata Makumbusho hiyo ya kisasa sio jambo dogo na kuongeza kuwa itasaidia kufungua fursa za kiuchumi katika jamii hiyo.
Amefafanua kuwa moja ya shabaha ya Serikali ya kuzindua Makumbusho hiyo ni kuhakikisha fursa za kiuchumi zinatapakaa kila pembe ya nchi ili kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya utalii.
Kufuatia hatua hiyo, Mwenyekiti Mabeyo ameiagiza Menejimenti ya NCAA kuendelea kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya utalii katika eneo hilo la Kimondo ili watalii wakija eneo hilo wakute vitu vingi vya kutembelea.
Hata hivyo ametaja faida ya kutembelea vivutio vya utalii ni pamoja na kupata utulivu wa afya ya akili.
Vile vile Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa kimila kwa kutoa ushirikiano kuonesha mila na desturi ya jamii inayokaa katika maeneo hayo na kusema kuwa Makumbusho hiyo ni ya kwanza ya aina yake kwa Nyanda za Juu Kusini.
"Mahali hapa panahitaji kutunzwa kutokana na historia yake, hata jina la mkoa wa Songwe umetokana na uwepo wa ndege wakubwa wenye shingo ndefu walioitwa Songwesis" ameongeza Mwenyekiti Mabeyo.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amewapongeza wananchi wanaoishi katika eneo hilo kwa kukubali kutoa ardhi yao kwa ajili ya kuendeleza eneo hilo kiutalii.
"Serikali imekusudia kulipa Bil. 1.4 kwa wananchi waliopisha upanuzi wa kituo hiki hivyo naomba muendelee kuipenda selikali yenu kwa vile hadi sasa tumeshatenga kiasi cha fedha cha kuanza kulipa fidia hizo" amesisitiza Mabeyo
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael amewataka NCAA kuendelea kufanya maboresho zaidi katika kituo hicho cha Kimondo ili kuwavutia watalii wengi kutembelea eneo hilo.
Ametumia fursa hiyo kuwaita wawekezaji kwa kuzitaja fursa za uwekezaji katika eneo la maliasili na utalii katika mkoa huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli, kumbi za mikutano, kampuni za kitalii,ufugaji nyuki, bandari kavu, utalii wa madini na utalii.