MCHENGERWA AANZISHA RUFIJI STAR SEARCH, RUFIJI FM.

       


************************

👉Amshukuru Mhe. Rais, awaomba watanzania washiriki katika uhifadhi wa raslimali.

Na John Mapepele

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Mkoa wa Pwani na Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua rasmi kampeni maalum ya kusaka vipaji katika Jimbo hilo kwa lengo la kuzalisha na kuviendeleza vipaji lukuki vilivyomo katika jimbo hilo.

Mhe. Mchengerwa amezindua kampeni hiyo itakayojulikana kama Rufiji Star Search (RSS) usiku wa kuamkia leo kwenye Tamasha la uzinduzi wa kituo kipya cha Kisasa ya Redio Rufiji FM.

Akizindua kampeni hiyo katika Tamasha ambalo lilipambwa na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya na kujaza maelfu ya Wananchi kutoka Rufiji na mikoa jirani amefafanua kuwa msanii nguli nchini Mrisho Mpoto ndiye ataongoza jopo la majaji katika zoezi hilo la kusaka vipaji katika kata zote za Rufiji.

Amesema Rufiji ni miongoni mwa maeneo ambayo yamebarikiwa kuwa na vipaji vingi vya Sanaa lakini havijatambuliwa hivyo kampeni hii inakwenda kuvumbua vipaji hivyo.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo imetarajiwa kuwa endelevu ambapo kwa msimu huu wa awali watawachuja na kuwapata washindi kumi bora.

Amewataka vijana wenye uwezo kujitokeza na kujishindana vikali ili waweze kuonyesha uwezo wao hatimaye waweze kushinda na kubadilisha maisha yao kwani Sanaa ni mtaji na ajira.

Tamasha hilo la uzinduzi wa kituo hicho cha Redio cha Rufiji FM limeacha historia kwa kuwajaza maelfu ya Wananchi wa rika zote na wasanii wengi ambao waliisimamisha Rufiji kwa usiku wa kuamkia leo.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa kituo hicho pamoja na kutoa burudani nzito pia kitakumika kutoa taarifa za maendeleo ya wanaRufiji.

"Kama tunavyofahamu kazi za msingi za vyombo vya Habari ni kuelimisha, kuburudisha na kutoa taarifa, basi Redio hii itajikita zaidi katika maeneo hayo huku ikizingatia maadili ya kitanzania" amesisitiza Mhe Mchengerwa

Mhe. Mchengerwa ametumia Tamasha hilo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya huduma za wananchi kama ujenzi wa shule, zahanati na barabara.

Pia katika usiku huo, ametoa hundi ya zaidi ya milioni 478 kwa kikundi cha Ushirika.

Katika hatua nyingine Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi wa Rufiji na watanzania wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhifadhi raslimali za nchi kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.

Post a Comment

Previous Post Next Post