TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inapenda kutoa ufafanuzi wa Habari iliyosambaa katika mitandaoni ya kijamii kuwa “Huduma ya Pace Maker haipo Muhimbili, Wagonjwa wanakufa” taarifa hiyo siyo ya kweli na ipuuzwe, kwani hakuna mgonjwa aliyekufa kutokana na tatizo la kutokuwekewa kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri “Pacemaker”.
Taasisi ilikuwa na upungufu wa Pacemaker kwa muda wa wiki mbili ilitokana na mtoa huduma ya kusambaza vifaa hivyo kuchelewa kuvileta hapa nchini kutoka nchini Uholanzi. Hata hivyo, iwapo inatokea upungufu wa vifaa hivi Taasisi inautaratibu wa kuhifadhi vichache kwa ajili ya kutumika kwa wagonjwa wa dharura kwani wagonjwa wanaowekewa Pacemaker wako wa aina mbili kuna wa dharura na wale wanaoweza kusubiri.
Kutokana na changamoto hii wagonjwa wote waliokuwa wa dharura waliwekewa Pacemaker ambapo kwa wiki ya tarehe 06-12/2/2023 wagonjwa watatu waliwekewa kifaa hicho. Wiki ya tarehe 13-19/02/2023 hakukuwa na mgonjwa wa dharura aliyehitaji kuwekewa Pacemaker.
Siku ya jana tarehe 23/2/2023 Taasisi ilipokea Pacemaker kutoka kwa mtoa huduma ya kusambaza vifaa hivyo na siku ya jana wagonjwa watatu waliwekewa kifaa hicho na leo tarehe 24/02/2023 wagonjwa watano wanawekewa pia wanaohitaji kuwekewa Pacemaker wamepewa taarifa kufika Hospitali.
Aidha, endapo itatokea Taasisi ikaishiwa kabisa Pacemaker ingawa haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, kuna utaratibu ambao umewekwa wa kuazima vifaa hivyo kutoka Hospitali za hapa nchini na Afrika ya Mashariki ambazo zinatoa huduma ya upasuaji wa moyo.
Taasisi inatoa onyo kwa watu waliotoa taarifa hii ya uongo ambayo imezua sintofahamu kwa wananchi pamoja na wagonjwa wetu kuacha mara moja kufanya hivyo. Tunaendelea kusisitiza iwapo mtu anahitaji kupata ufafanuzi kuhusu huduma zetu au anakutana na changamoto yoyote ile ya kimatibabu afike katika Taasisi yetu au apige simu namba +255688027982 au +255782042019 kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi.
“Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”.
Madaktari bingwa wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) Tulizo Shemu na Yona Gandye wakimwekea mgonjwa kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri (Pacemaker) leo tarehe 24/02/2023